Iran: Mazungumzo yajayo ya Vienna sharti yawe na tija ya maana
(last modified Wed, 06 Oct 2021 13:07:09 GMT )
Oct 06, 2021 13:07 UTC
  • Iran: Mazungumzo yajayo ya Vienna sharti yawe na tija ya maana

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema duru ijayo ya mazungumzo ya Vienna yanayolenga kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA inapasa iwe na matokeo ya maana na yenye kutekelezeka.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo baada ya kuwasili Moscow, alikoenda kufuatia mualiko wa mwenzake wa Russia, Sergei Lavrov na kubainisha kuwa, iwapo mazungumzo hayo yatafuata njia iliyofuatwa miaka minane iliyopita, bila shaka Iran itachukua uamuzi muafaka wakati huo, na kwa kuzingatia fremu maalumu.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa, "Iwapo tutafikia tija ya maana katika kulinda haki za Wairani kwenye mazungumzo yajayo ya Vienna na washirika wengine, makubaliano hayo yatakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha mpango wa serikali ya (Rais Ibrahim) Raisi (wa Iran) wa ustawi endelevu wa uchumi."  

Kikao cha nyuma cha Vienna, mji mkuu wa Austria

Hadi sasa zimeshafanyika duru sita za mazungumzo huko mjini Vienna kwa madhumuni ya kuirejesha Marekani kwenye utekelezaji wa makubaliano hayo ya nyuklia, mazungumzo ambayo yamehudhuriwa na nchi zilizosalia katika JCPOA.

Tehran inasisitiza kuwa, kibali cha kuirejesha Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kuhakikisha nchi hiyo inaondoa vikwazo vyote haramu vipatavyo 800 ilivyoiwekea Iran katika utawala wa Donald Trump.

Tags