Iran: Mabadilishano ya wafungwa yasihusishwe na mazungumzo ya JCPOA
(last modified Tue, 19 Oct 2021 13:28:12 GMT )
Oct 19, 2021 13:28 UTC
  • Iran: Mabadilishano ya wafungwa yasihusishwe na mazungumzo ya JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran inalitazama suala la kubadilishana wafungwa kuwa la kibinadamu, na haitaki kuona likifungamanishwa na mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, Iran inakaribisha mazungumzo yatakayokuwa na tija, na ipo kurejea katika utekelezaji wa majukumu yake iwapo upande wa pili pia utatekeleza wajibu wake.

Ameashiria mazungumzo ya JCPOA na kueleza kuwa, majadiliano yaliyofanyika karibuni baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Ali Bagheri Kani na Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya kigeni, yalikuwa chanya na yataendelea wiki ijayo mjini Brussels.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran sambamba na kugusia kuhusu wimbi la mashambulizi ya kigaidi dhidi ya waumini wakiwa katika sehemu za ibada huko Afghanistan, amemtaka mkuu wa UN achukue hatua za makusudi kupambana na zimwi la ugaidi nchini humo.

Mazungumzo ya nyuma ya JCPOA mjini Vienna

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, Umoja wa Mataifa unapawa kuwajibika wakati huu kuliko wakati wowote ule, kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi wanaomiminika nchini Iran wakitokea Afghanistan.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo utaendelea kuwapa wananchi wa Afghanistan misaada ya kibinadamu, huku akisisitizia haja ya kuundwa serikali jumuishi katika nchi hiyo.

Kadhalika amesema UN inaunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na unaitakia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kila la kheri katika mazungumzo ya kujaribu kuyahuisha mapatano hayo ya kimataifa.

Tags