Iran: Kundi la 4+1 liwe tayari kwa mazungumzo yatakayoheshimu haki
(last modified Tue, 02 Nov 2021 14:41:50 GMT )
Nov 02, 2021 14:41 UTC
  • Iran: Kundi la 4+1 liwe tayari kwa mazungumzo yatakayoheshimu haki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kundi la 4+1 lililosalia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA linapaswa kujiandaa kwa mazungumzo ya kuhuisha mapatano hayo ya kimataifa, kwa kuzingatia na kuheshimu misingi ya haki na maslahi ya pande zote.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hayo leo Jumanne katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa: Ikulu ya White House inaitisha mazungumzo na Iran na kudai kuwa iko tayari kurejea katika makubaliano ya JCPOA, lakini wakati huohuo, inatangaza vikwazo vipya dhidi ya maafisa na taasisi za Iran.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia kwa karibu mienendo ya Rais Joe Biden wa Marekani na kusisitiza kuwa, mazungumzo yanapaswa kufanyika kwa dhati na si kwa sababu tu yafanyike.

Trump aliyeiondoa Marekani katika JCPOA mwaka 2018

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa, lengo la mazungumzo ni kufikiwa makubaliano ya maana kwa misingi ya kuheshimu maslahi ya pande husika.

Mnamo Mei mwaka 2018, Marekani kupitia rais wa wakati huo Donald Trump ilikiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kujiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kinyume cha sheria.

Tags