"Iran inataka 'makubaliano mazuri' katika mazungumzo ya Vienna"
(last modified Thu, 11 Nov 2021 08:13:05 GMT )
Nov 11, 2021 08:13 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili limejiandaa kwa ajili ya kufikiwa 'makubaliano mazuri' katika mazungumzo ya Vienna kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA, yanayotazamiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana usiku na kuongeza kuwa, "katika meza ya mazungumzo huko Vienna, tupo tayari kufikiwa mapatano mazuri."

Waziri Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, mazungumzo hayo ya kujaribu kuhuisha utekelezaji wa JCPOA yatazaa matunda iwapo pande zote husika zitarejea katika utekelezaji wa majukumu yao.

Sambamba na kusisitizia udharura wa kuondolewa Tehran vikwazo vyote haramu mara moja, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amefafanua kuwa, sharti Jamhuri ya Kiislamu ipate dhamana ya kutekelezwa kivitendo nukta zote zitakazoafikiwa kwenye mazungumzo hayo yanayotazamiwa kuanza tena mwishoni mwa mwezi huu.

Mazungumzo ya Vienna kuanza tena Novemba 29

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema naibu wake, Ali Baqeri amezitembelea nchi kadhaa za Ulaya na kufanya mazungumzo ya kufana na maafisa wa nchi hizo.

Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, kufikia sasa, Baqeri amezitembelea Ujerumani na Ufaransa, na anatazamiwa kuitembelea Uingereza leo Alkhamisi.

Vikao vya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyoingia kwenye kinamasi baada ya Marekani kujiondoa kwayo mwaka 2018, vinatazamiwa kuanza tena Novemba 29 huko Vienna nchini Austria.

Tags