Iran: Tuna nia njema tunapoingia kwenye mazungumzo ya Vienna
(last modified Sun, 14 Nov 2021 08:18:35 GMT )
Nov 14, 2021 08:18 UTC
  • Iran: Tuna nia njema tunapoingia kwenye mazungumzo ya Vienna

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii ina azma na nia njema inapojiandaa kuingia katika duru mpya ya mazungumzo ya Vienna kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mkutano wake wa jana jioni na kundi la wahadhiri na maprofesa wa Vyuo Vikuu, wanaharakati, waandishi wa habari, mabalozi na wachambuzi wa mambo na kusisitiza kuwa, sera ya Tehran ni kuona kuwa tija ya mazungumzo hayo ni kuondolewa vikwazo haramu, visivyo vya kiadilifu na vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Wairani.

Amesema katika sera za nje ya serikali ya awamu ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni kurejea Iran kwa nia njema kwenye mazungumzo ya Vienna, licha ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria kwenye mapatano ya JCPOA, na kutochukua hatua za maana za kutekeleza wajibu wao nchi za Ulaya. 

Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, mazungumzo hayo ya kujaribu kuhuisha utekelezaji wa JCPOA yatazaa matunda iwapo pande zote husika zitarejea katika utekelezaji wa majukumu yao, na Iran iondolewe vikwazo vyote haramu tena bila masharti.

Mazungumzo ya Vienna nchini Austria

Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter hivi karibuni, mwanadiplomasia huyo wa Iran alisisitiza kuwa, "katika meza ya mazungumzo huko Vienna, tupo tayari kufikiwa mapatano mazuri."

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa, Ali Bagheri Kani ambaye pia alihudhuria mkutano huo wa jana amefafanua kuhusu nafasi na hatua ilizochukua Iran katika uwanja huo.  Vikao vya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyoingia kwenye kinamasi baada ya Marekani kujiondoa kwayo mwaka 2018, vinatazamiwa kuanza tena Novemba 29 huko Vienna nchini Austria.

 

Tags