Iran haitaki makubaliano ya muda, yataka vikwazo viondolewe kwa mkupuo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, vikwazo vyote haramu vya Marekani dhidi ya taifa la Iran vinapaswa kuondolewa kwa mkupuo, na kwamba Tehran katu haitakubali 'makubaliano ya muda' kwenye mazungumzo ya Vienna ya kujadili makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, yanayoanza ndani ya siku chache zijazo.
Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Ijumaa na kueleza kuwa, vikwazo vyote vya Marekani vinapaswa kuondolewa mara moja na si hatua kwa hatua, ikisisitiza kuwa Washington inapaswa kutoa dhamana kwamba haitaondoka tena kwenye mapatano hayo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa kauli hiyo kufuatia ripoti za baadhi ya vyombo vya habari kuhusu pendekezo la Wamagharibi la kutaka vikwazo dhidi ya Iran viondolewe hatua kwa hatua.
Khatibzadeh amebainisha kuwa, Iran inaingia katika mazungumzo ya Vienna ikiwa na azma thabiti ya kuondolewa taifa hili vikwazo vyote vya kidhalimu kwa mkupuo, kisha Jamhuri ya Kiislamu ijiridhishe kuwa vikwazo hivyo vimeondolewa kivitendo.
Mashirika ya habari ya Marekani haswa gazeti la New York Times katika siku za hivi karibuni yameeneza habari kwamba Washington inapania kuondoa sehemu ya vikwazo dhidi ya Iran mkabala wa Tehran kusimamisha baadhi ya shughuli zake za miradi ya nyuklia.
Aidha wiki iliyopita, shirika la habari la Axios la Marekani liliripoti kuwa, Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani alimuambia mwenzake wa Israel kuwa, Washington inataka kufikiwa makubaliano ya muda katika mazungumzo ya Vienna ili kwa utaratibu huo, kuandaa mazingira ya kufanyika vikao virefu vya kuipoteza muda Iran.