Burkina Faso yaomba uzoefu wa Iran katika mapambano dhidi ya ugaidi
Waziri mpya wa Mambo ya nje wa Burkina Faso ameiomba Iran, kama nchi ambayo imeathiriwa na ugaidi kwa miaka mingi, kuipatia Ouagadougou uzoefu wake katika uwanja huo.
Shirika la Habari la Iran IRNA limeripoti mapema leo Jumanne kwamba, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amasema Tehran imeazimia kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ikiwemo Burkina Faso.
Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, Olivia Rouamba, akiangazia umuhimu wa Afrika katika malengo ya sera ya kigeni ya Tehran.
Vilevile ameeleza wasiwasi wake kuhusu harakati za makundi ya kigaidi ya kitakfiri nchini Burkina Faso na Afrika Magharibi kwa ujumla.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amempongeza Olivia Rouamba kwa kuteuliwa kuwa Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso na kumtakia mafanikio katika nafasi yake mpya.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Burkina Faso ameiomba Iran, kama nchi ambayo imeathiriwa na ugaidi kwa miaka mingi, kuipatia Ouagadougou uzoefu wake katika uwanja huo.
Olivia Rouamba ametoa wito wa kuongezwa ushirikiano wa kisayansi na kiufundi baina ya nchi hizo mbili na vilevile msaada wa Iran katika nyanja mbalimbali.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Burkina Faso amewapongeza Wairani na Waislamu kwa mnasaba wa kuwadia mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.