Kiongozi Muadhamu: Kuwa na uhusiano na Wazayuni ni kosa kubwa sana
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na ambayo kwa mwaka huu yanasadifiana na Ijumaa ya keshokutwa ya tarehe 29 Aprili, 2022 na kusema kuwa, kuwa na uhusiano na utawala huo dhalimu ni kosa kubwa sana.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema hayo jana jioni wakati alipoonana na wanafunzi wa vyuo vikuu na wawakilishi wa vyama vya wanachuo kutoka kona zote za Iran na kusisitiza kuwa, kwa kutilia maanani kujitolea kukubwa wanakafanya wananchi wa Palestina na jinai kubwa mno za Wazayuni, Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu itaadhimishwa kwa shauku na hamasa kubwa zaidi kuliko miaka iliyopita. Amesema, inabidi kutangaza kwa sauti kubwa mshikamano na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina lakini waliosimama imara katika kupambana na dhulma ili kuwaongezea nguvu na moyo wa kuzidi kuwa imara.
Aidha amesema, Siku ya Kimataifa ya Quds ni fursa nzuri ya kutangaza mshikamano na wananchi wa Palestina na amezilaumu vikali zile nchi ambazo zinashirikiana na Wazayuni katika jinai zao. Amesema: Inasikitisha kuwa serikali za nchi za Waislamu zimechukua hatua mbaya mno. Haziko tayari hata kuzungumzia kwa maneno tu kadhia ya Palestina na baadhi ya serikali hizo zinadhani kwamba, njia ya kuisaidia Palestina ni kuwa na uhusiano wa kawaida na Wazayuni katika hali ambayo hilo ni kosa kubwa sana.
Kiongozi Muadhamu amekumbusha uzoefu mchungu wa huko nyuma na kuhoji kwa kusema: Hivi kwani Misri haikuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni? Je, uhusiano huo umepunguza jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina? Je, uhusiano baina ya Misri na utawala wa Kizayuni, umeweza kupunguza kuvunjiwa heshima Msikiti wa al Aqsa? Mbona hivi sasa baadhi ya serikali za nchi za Waislamu zinataka kurejea kosa hilo hilo la Anwar Saadat?
Matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yamezilenga tawala za baadhi ya nchi za Kiarabu na za Waislamu ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimejiingiza kwenye mkumbo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kwa amri ya Marekani. Nchi hizo zimejifanya kutoona jinai kubwa na malengo ya kupenda kujitanua utawala wa Kizayuni na huo kwa hakika ni usaliti mkubwa kwa kadhia nzima ya Palestina.
Licha ya makubalino ya nchi za Kiarabu ya kuheshimu kikamilifu malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina, lakini nchi za Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain, Sudan na Morocco ziliamua kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni katika kipindi cha baina ya miezi ya Septemba hadi Disemba 2020.
Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kuwa, utawala wa Kizayuni una historia ndefu mbaya ya kukalia kwa mabavu ardhi za Waislamu na kutenda jinai dhidi ya binadamu na hususan dhidi ya taifa la Palestina. Hakuna wakati wowote ambapo utawala wa Kizayuni umewahi kuwa na nia njema au angalau kuonesha nia njema kwa mataifa ya Waislamu kwenye eneo hili. Muda wote utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha siasa zake za kujitanua, kukalia kwa mabavu ardhi za Waislamu, kufanya jinai dhidi ya Waislamu na baya zaidi ni kwamba katika mwezi huu wa Ramadhani, wanajeshi wa utawala dhalimu wa Israel wamefanya jinai kubwa sana ndani ya Msikiti wa al Aqsa ambazo hazijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha mwaka mzima uliopita. Katika jinai yao hiyo, Wazayuni walipiga mabomu ndani ya Msikiti wa al Aqsa, wakawajeruhi Waislamu 350 waliokuwa kwenye ibada ndani ya Ramadhani na kuwateka nyara Wapalestina wengine wasiopungua 400.
Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasisitiza kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni kosa kubwa sana. Lakini pia amesema, wananchi na vijana wa Palestina wamesimama imara kupambana na jinai za utawala wa Kiayuni. Aidha amemuomba Mwenyezi Mungu atie taufiki katika mapambano ya Wapalestina hadi ukombozi kamili wa Palestina na Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.