Wanafunzi Tehran walaani mauaji ya mwandishi habari Mpalestina Abu Akleh
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i83562-wanafunzi_tehran_walaani_mauaji_ya_mwandishi_habari_mpalestina_abu_akleh
Wanafunzi wa vyuo vikuu katika mji mkuu wa Iran, Tehran wameandamana nje ya Ubalozi wa Palestina na kuulaani utawala haramu wa Israel kwa kumuua kinyama mwandishi habari Mpalestina wa Televisheni ya Al Jazeera Shireen Abu Akleh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2022 03:25 UTC
  • Wanafunzi Tehran walaani mauaji ya mwandishi habari Mpalestina Abu Akleh

Wanafunzi wa vyuo vikuu katika mji mkuu wa Iran, Tehran wameandamana nje ya Ubalozi wa Palestina na kuulaani utawala haramu wa Israel kwa kumuua kinyama mwandishi habari Mpalestina wa Televisheni ya Al Jazeera Shireen Abu Akleh.

Wanafunzo hao wa vyuo vikuu kutoka Iran, Lebanon na Palestina walijumuika pia kumuenzi shahidi Abu Akleh.

Mapema Jumatano, mwandishi wa habari ya televisheni ya al Jazeera, Shireen Abu Akleh, 51, alipigwa risasi na kuuliwa shahidi kikatili na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakati akiwa kwenye kazi yake ya kuripoti uvamizi wa kijeshi wa jeshi la Israel katika kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Jenin.

Jinai hiyo inaendelea kulaaniwa kimataifa huku watetezi wa haki za binadamu wakitaka utawala huo wa Kizayuni ufikishwe kizimbani.

Mjumuiko wa kumuenzi Shahidi Shireen Abu Akleh mjini Tehran

Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali jinai hiyo na kusema kuwa, utawala ghasibu wa Israel una hofu na woga wa kutangazwa habari sahihi na za kweli.

Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia ya shahidi huyo na taifa la Palestina amesema kuwa, hatua hii ya kijinai ya Israel ni ushahidi wa wazi kwamba, utawala huo ghasibu hauheshimu kabisa tasnia ya habari.

Naye Lolwah Alkhater Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amelaani kitendo cha utawala ghasibu wa Israel cha kumuua mwandishi huyo wa habari huku akitoa wito wa kuhitimishwa 'ugaidi wa kiserikali wa Israel.' Aidha amesema kuna wajibu wa kukomeshwa uungaji mkono usiohoji kitu kwa Israel.