Kituo cha Kistratijia cha 313; Nembo ya Uwezo wa Kijeshi wa Iran
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri siku ya Jumamosi alikagua kituo kipya cha siri kilicho chini ya ardhi cha ndege zisizo na rubani cha Jeshi la Jamhuri Kiislamu ya Iran. Akiwa hapo alijioenea uwezo mkubwa wa ndege za kivita zisizo na rubani za jeshi hilo zilizoko katika kituo hicho cha siri.
Aidha alishuhudia kuanza kazi kituo cha aina yake cha ndege zisizo na rubani ambacho kiko mamia ya mita chini ya ardhi na ambacho sasa ni nembo ya uwezo na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa ndege za kivita zisizo na rubani au drone.
Admeri Mousavi, Mkuu wa Kitengo cha Oparesheni katika Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akizungumza Jumamosi katika mahojiano na Kanali ya Kwanza ya Televisheni ya Iran kuhusu kituo hicho kikubwa cha ndege zisizo na rubani kilichopewa jina la "Kituo cha Kistratijia cha 313" alisema: "Aina ya ndege zisizo na rubani katika kituo hiki zinaweza kutekeleza oparesheni zenye taathira kubwa ili kuweza kulenga nguzo kuu na muhimu za adui katika mapigano."
Amesema kituo hicho kina aina mbali mbali mbali za ndege zisizo na rubani zikiwemo zile zenye magurudumu zinazoruka kama ndege za kawaida za kivita na pia zenye kuvurumishwa kama makombora.
Ustawi wa Iran katika uga wa ndege zisizo na rubani umekuwa wa aina yake katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Ndege za kivita zisizo na rubani zilizoundwa Iran zimeweza kutumika katika muongo mmoja uliopita ambapo zimeweza kuonyesha uwezo wake mkubwa katika oparesheni za upelelezi, ushambuliaji na ulengaji shabaha kwa umakini mkubwa.
Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameweza kupata mafanikio makubwa sana katika teknolojia ya utengenezaji ndege za kivita zisizo na rubani na hivi sasa nchi hii imebadilika na kuwa dola lenye uwezo mkubwa zaidi katika uga wa ndege zisizo na rubani katika eneo.
Ndege zisizo na rubani za Iran zina uwezo wa kulinda asalama na mipaka ya nchi hii kwa kuruka maelfu ya kilomita nje ya mipaka ya nchi kavu na baharini. Katika miaka ya hivi karibuni Iran imejikita katika kuimarisha uwezo wa kiteknolojia wa ndege zake zisizo na rubani na sambamba na hilo pia imeweza kuzizalisha kwa wingi na leo nchi hii ina nafasi ya kipekee duniani miongoni mwa nchi zinazomiliki teknolojia ya kisasa ya kuunda ndege zisizo na rubani.
Aidha Jumamosi Jeshi la Iran pia lilizindua kombora la cruise lijulikanalo kama Heidar 1 lenye uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 200 kwa kasi ya kilomita 1000 kwa saa. Kombora la Heidar 1 linaweza kuvurumishwa kutoka katika ndege isiyo na rubani. Jeshi la Iran pia limezindua kombora jingine lijulikanalo kama Heidar 2 ambalo linaweza kuvurumishwa kutoka katika helikopta.
Admeri Mousavi anasema: "Uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa ndege zisizo na rubani sambamba na uwezo katika makombora ni nguzo mbili muhimu ambazo zinalipatia jeshi nguvu za kuuhami mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."
Hivi sasa baada ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuzindua kituo kipya cha siri kilicho chini ya ardhi chenye idadi kubwa ya ndege za kisasa za kivita zisizo na rubani, uwezo mkubwa wa Iran katika ndege zisizo na rubani umeweza kubainika wazi.
Kwa kuzingatia vita vya hivi karibuni duniani kama vile vita vya Nagorno-Karabakh na vita vya Ukraine, imefahamika zaidi kuwa ndege zisizo na rubani zina nafasi muhimu sana katika oparesheni za upelelezi na ujasusi na kuongoza vikosi vya nchi kavu katika medani ya vita na hatimaye kungamiza ngome za adui.
Kwa msingi huo Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuzingatia utambulisho wa mbinu mpya za kivita imechukua mkondo wa kuimarisha uwezo wa nchi hii katika sekta ya ndege zisizo na rubani.
Katika vita vya kisasa, oparesheni mbali mbali za kujihami na kuvamia zikiwemo za nchi kavu, angani na baharini na pia katika vita vya kielektoroniki hutegemea sana ndege zisizo na rubani.
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri anasema katika vita vya hivi karibuni eneo la Caucasia, na Ukraine na maeneo mengine duniani na hali kadhalika katika vita dhidi ya magaidi huku Iraq, Syria na Nigeria, ndege zisizo na rubani zimekuwa na nafasi ya kipekee na utumizi wa ndege hizo unazidi kuongezeka. Kwa kudiriki hitajio la vita vya mustakabali na kwa kutumia mbinu za kisasa kabisa, Jeshi la Iran linajizatiti kwa silaha za kisasa kabisa na kwa bahati nzuri leo tumeona uwezo mkubwa wa ndege za kivita katika jeshi.