Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la kurejeshwa nyuma na Iran Uistikbari wa dunia
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ikipata ilhamu ya Ahlul-Beiti (as) iliyashinda na kuyarejesha nyuma majoka yenye vichwa saba ya Uistikbari na ikasonga mbele kimaendeleo.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema hayo Jumamosi ya jana tarehe tatu Septemba alipoonana na wajumbe wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Beiti (as) pamoja na wageni washiriki wa mkutano wa 7 jumuiya hiyo na kueleza kwamba, adhama na kupendwa Ahlul-Beiti (watu wa nyumba ya Bwana Mtume) katika Ulimwenguu wa Kiislamu ni jambo lisilo na mithili. Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kuwa, kushajiisha mataifa mengine kusimama kidete mbele ya vitendo vya utumiaji mabavu ni moja ya sababu za uadui za mfumo wa kibeberu na uadui wao dhidi ya Iran na kubainisha kwamba, kusambaratishwa njama za kijinai za Marekani katika mataifa mbalimbali ambapo mfano wa wazi ni kutokomezwa kundi la kigaidi la Daesh, ni moja ya mambo yaliyowafanya maadui kuelekeza nguvu zao katika kuionyesha Iran kuwa ni tishio na kuituhumu kwamba, eti inaingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine.
Moja ya engo nyingine muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kusisitiza kuuchukia ubeberu na Uistikbari ambalo mbali na kubainishwa wazi katika Katiba, katika kipindi cha miongo minne iliyopita, hilo limekuwa ni katika vipaumbele vya sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa kuzingatia umuhimu wa kuchukia uistikabri na kupinga satuwa ya ajinabi, jambo hili limetiliwa mkazo pia katika kipengee cha 152 cha katiba.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameingiza neno katika uga wa fasihi ya siasa ulimwenguni ambalo sifa yake maalumu ni kuwa roho na moyo wa kupigania mamlaka ya kujitawala na kuchukia ubeberu. Neno uistikbari ambalo limekaririwa katika fasihi ya kisiasa ya Mapinduzi ya Kiislamu chimbuko lake ni mafundisho ya Qur’ani Tukufu. Neno hili lina maana ya kuonyesha ukubwa na kuwa juu kwa wengine na kujiona kwamba, wewe ndiye mdhibiti na unayehodhi mambo.
Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa akisisitiza mno juu ya kuchukia ubeberu ambapo nembo ya hilo ni kupambana kwake na siasa na hatua za Marekani ikiwa shetani mkubwa na dhihirisho la uistikbari katika zama za leo. Katika kipindi chote cha miongo minne ya hivi karibuni daima tumeshuhudia hatua za chuki na uadui pamoja na ushari wa Marekani dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kiasi kwamba, Washington ikiwa kinara wa kambi ya Magharibi imetumia suhula na nguvu zake zote kwa ajili ya kuendesha njama dhidi ya mfumo huu.
Imam Khomeini akiwa na ufahamu kamili wa utambulisho wa uistikbari wa Marekani alitahadharisha mara chungu nzima kuhusiana na hilo na alisisitiza juu ya kuweko mapambano athirifu dhidi ya serikali ya Washington. Aidha Imam Khomeini alikuwa akiamini kwamba, hatua ya chuki ya Uislamu dhidi ya uistikbari iliyopelekea kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu, haiishii tu katika jiografia ya Iran bali hilo ni jambo ambalo linapaswa kuweko katika maeneo yote ya wanyonge na wastadhaafu. Kati ya malengo ya juu ya Mapinduzi ya Kiislamu, suala la chuki dhidi ya uistikabri lina nafasi maalumu.
Utendaji wa Iran wa chuki dhidi ya ubeberu katika kipindi cha uongozi wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran umefuatiliwa kwa nguvu zote. Mfano wa wazi wa hilo ni kukabiliana na mikakati ya kibeberu ya Marekani kama vile mpango wa Mashariki ya Kati Kubwa katika kipindi cha uraia wa George W. Bush, himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa makundi ya kigaidi kama Daesh kwa ajili ya kuzusha fitina katika eneo katika kipindi cha urais wa Barack Obama na vilevile mpango mchafu wa Abraham wenye lengo la kutaka kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya mataifa ya eneo na utawala ghasibu wa Israel katika kipindi cha urais wa Donald Trump. Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, Marekani imetekeleza njama na mipango mbalimbali tena kwa mbinu tofauti kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la malengo yake. Jambo jingine ni hatua ya Washington ya kuanzisha muungano katika eneo dhidi ya Iran sambamba na kuhaha huku na kule kueneza propaganda za kutaka kuionyesha Iran kwamba, ni tishio. Utawala haramu wa Israel ukiwa muitifaki wa kiistratejia wa kieneo wa Marekani ni mshirika mkuu wa njama na mipango ya kiistikbari.
Mkabala na mipango hii ya kiistikbari, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikitumia tadibiri na mipango madhubuti na kwa himaya na uungaji mkono wa waitifaki wake wa eneo imefanikiwa kusambaratisha njama za Washington. Kuhusiana na hilo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiingilii masuala ya ndani ya mataifa mengine anasema kuwa, tuhuma hizo chimbuko lake ni kushindwa kwao katika kuzuia ustawi na maendeleo makubwa ya mfumo wa Kiislamu; ingawa watu wote wanapaswa kuwa macho mbele ya siasa za kibeberu na kutofuata siasa hizo.
Jambo jingine ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelisisitizia ni ulazima wa kuwa macho mataifa ya Kiislamu mbele ya njama na mipango michafu ya maadui wa Uislamu na Waislamu ya kuleta mifarakano hususan ile inayofuatiliwa na Marekani.
Ayatullah Khamenei amesema: Sera za hivi sasa za uistikbari ni kukuza tofauti na hilafu na kuchora mistari isiyo na ukweli katika ulimwengu wa Kiislamu na kubainisha kwamba: Uchochezi na kupanga mipango ya kuzusha vita baina ya Mashia na Masuni, Waraabu na wasiokuwa Waarabu, Shia na Shia na Suni na Suni ni mambo ambayo hivi sasa yanashuhudiwa katika baadhi ya nchi, hivyo kuna haja ya kuwa macho na kukabiliana na siasa za shetani mkubwa yaani Marekani.