Kutumiwa siasa na Magharibi katika suala la haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i90494-kutumiwa_siasa_na_magharibi_katika_suala_la_haki_za_binadamu
Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ambaye pia na Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Idara ya Mahakama ya Iran amesema, inasikitisha kwamba leo hii haki za binadamu zinatumiwa zaidi kisiasa kuliko ilivyowahi kuwa wakati wowote ule.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 13, 2022 22:52 UTC
  • Kutumiwa siasa na Magharibi katika suala la haki za binadamu

Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ambaye pia na Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Idara ya Mahakama ya Iran amesema, inasikitisha kwamba leo hii haki za binadamu zinatumiwa zaidi kisiasa kuliko ilivyowahi kuwa wakati wowote ule.

Kazem Gharibabadi, ameyasema hayo katika mazungumzo na waandishi wa habari mjini New York na akaongezea kwa kusema: "Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zinazojiona kuwa ni wabeba bendera ya kutetea haki za binadamu zinahusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya ardhi zao wenyewe au katika nchi zingine duniani; kwa hivyo nchi hizo haziwezi kwa namna yoyote ile kuwa na ustahiki wa kuwa wabeba bendera katika uga wa haki za binadamu". 

Kazem Ghariabadi

Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Idara ya Mahakama ya Iran amebainisha kuwa: "hivi karibuni, kufuatia fujo na machafuko yaliyozushwa katika baadhi ya miji ya Iran, nchi za Magharibi zilinadi tena wito wa kuunga mkono haki za binadamu za wananchi wa Iran, ilhali maisha ya mamilioni ya Wairan haohao yameathirika vibaya sana kutokana na vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na Marekani".

Matamshi ya Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Idara ya Mahakama ya Iran yametolewa katika hali ambayo, katika wiki za karibuni na kufuatia uvurugaji wa amani uliofanywa katika baadhi ya miji ya Iran, nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, Canada na baadhi ya nchi za Ulaya kama Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zililitumia tena suala la haki za binadamu kama wenzo na kisingizio cha kuiwekea vikwazo vingine vipya ya kiuchumi na kisiasa Iran na kukoleza moto wa machafuko hapa nchini.

Tajiriba ya miongo ya hivi karibuni inaonyesha kwa uwazi kabisa jinsi nchi za Magharibi zinavyolitangaza suala la haki binadamu kwa kutumia vipimo vyao wenyewe na kwa malengo yao ya kisiasa; wakati ukweli ni kwamba, nchi hizo zina rekodi mbaya na mafaili machafu kuhusiana na haki za binadamu ndani ya jamii zao wenyewe na katika nchi zingine pia. 

Ukandamizaji wa raia wa polisi wa Marekani

Kwa kutoa mfano, wakati nchi hizo zinadai kutetea haki za wanawake na hivyo kuchochea na kukoleza moto wa machafuko katika baadhi ya miji ya Iran, zimefumbia macho ukweli mchungu na wa kusikitisha unaoshuhudiwa ndani ya jamii zao wenyewe; kwa sababu kulingana na takwimu zilizopo, kuna ukiukaji mkubwa wa haki za wanawake huko Magharibi. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa, Marekani ni nchi ya tatu duniani kwa matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono. Katika kila wanawake watatu wa Kimarekani, mmoja wao ameshawahi kufanyiwa unyanyasaji wa kingono katika maisha yake. Na hii ni katika hali ambayo, asilimia 62 ya ukatili wa kingono unaofanywa hauripotiwi kwa polisi ya Marekani na asilimia 92 ya wabakaji na wanyanyasaji wa kingono hawakai jela hata kwa muda wa siku moja.

Nukta nyingine muhimu kuhusu utendaji wa nchi za Magharibi katika uga wa haki za binadamu ni kwamba, nchi hizo ndizo wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu kutokana na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Iran, ambavyo hata vimepelekea wagonjwa wengi kufariki dunia kutokana na kukosa dawa wanazohitajia. Hadi sasa ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa ameshatoa ripoti kadhaa zinazoweka wazi mwenendo huo wa Wamagharibi unaokinzana na haki za binadamu. Alena Douhan alieleza yafuatayo alipojibu suali aliloulizwa kuhusu safari aliyofanya hapa nchini Iran ili kuchunguza athari hasi za hatua za mabavu za upande mmoja kuhusiana na haki za binadamu: "vikwazo vilikuwa na taathira kubwa hasi kwa mfumo wa afya; nilizungumza na wagonjwa wa kitengo cha dharura na watu wanaougua maradhi ya kijenetiki na saratani; matokeo yanaonyesha kuwa dawa zinazohitajika hazipatikani".

Alena Douhan

Ni wazi kwamba ufanyaji mambo kisiasa na uchukuaji hatua kimaslahi unaofanywa na nchi za Magharibi zinazojinasibu kuwa watetezi wa haki za binadamu ndio kila mara unaosababisha madhara makubwa zaidi kwa haki zenyewe za binadamu. Wakati nchi hizo zinazodai kuwa watetezi wa haki za binadamu zinazipa uhalali wa kisheria hatua za kuwakandamiza wapinzani, kuwaua raia wao weusi bila hatia, kuwaua kwa halaiki raia wao wa jamii za waliowachache hususan Waislamu, kuwanyanyasa na kuwatesa wafungwa katika magereza yao na kuwataabisha wahajiri ndani ya mipaka yao, zinachukulia kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu hatua za kimahakama na utekelezaji wa sheria unaofanywa na Iran inayokabiliwa na vikwazo vya kiuchumi vya nchi hizohizo; na kujaribu kupindua ukweli wa mambo kupitia propganda kubwa na chafu za vyombo vyao vya habari.

Ni kutokana na yote hayo, ndipo Mkuu wa Masuala ya Kimataifa na Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran akasema, lengo la safari yake mjini New York ni kwenda kutoa picha na taswira sahihi kuhusu hali ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasisitiza kwa kusema: "tusiruhusu fikra za waliowengi katika nchi mbalimbali zipotoshwe na taswira potofu na ya uadui inayotolewa na nchi za Magharibi na Marekani".../