Brigedia Jenerali Salami: Ndoto za maadui kuhusu Iran hazitatimia
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesema kuwa wakuu wa Israel na Marekani wanahusika na ghasia na machafuko na wanaota ndoto nyingi kuhusu Iran ambazo hata hivyo hazitatimia.
Brigadia Jenerali Hussein Salami amesema katika mkutano wa vinara na wanajihadi wa uchumi wa kimuqawama katika mkoa wa Farsi kusini mwa Iran kwamba, leo hii Iran ya Kiislamu imepiga hatua za kimaendeleo chini ya uongozi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na adui hataki kuona wananchi wakiwa na amani. Ameongeza kuwa, miradi mbalimbali imekuwa ikitekelezwa na kufunguliwa hapa nchini ambapo adui anataka kuona Iran ikitawaliwa na uharibifu lakini licha ya matakwa hayo Iran ya Kiislamu imeibuka na kudhihirika kuwa nchi yenye nguvu kimataifa.
Brigedia Jenerali Salami ameeleza kuwa, maadui wamekuwa wakikimbia huku na kule duniani na sasa wamekumbwa na wasiwasi mkubwa. Ameongeza kuwa, watawala wa Israel na Marekani wanazungumzia uhuru wa Iran na kuingilia wazi masuala ya ndani ya nchi hii huku wakihusika na kuwa na nafasi ya kwanza katika machafuko ya hivi karibuni hapa nchini; hata hivyo taifa la Iran liko imara, limetoa mashahidi na halikujiunga na mrengo huo wa Marekani; na watu wetu wanajua vyema nini ndoto ya Marekani kwa Iran. "Adui anaota ndoto nyingi kuhusiana na Iran lakini kamwe ndoto hizo hazitatimia", amesema Brigedia Jenerali Hussein Salami.
Wakati huo huo Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ameashiria njama za adui kwa vijana wa Kiirani na kueleza kuwa, maadui wanataka vijana wetu watawaliwe na fikra za Kimagharibi, na wasikilize na kufuata bwabwaja na matakwa yao tu; adui hataki kuona Iran inakuwa na amani.