Hassan Qomi: Iran inashirikiana na serikali ya muda ya Taliban nchini Afghanistan
Mjumbe Maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Masuala ya Afghanistan ameeleza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashirikiana na serikaliya muda ya Taliban katika nyanja mbalimbali ikiwemo nyanja ya kiuchumi kwa kuzingatia siasa za kuwasaidia wananchi wa Afghanistan.
Shirika la habari la TASNIM limeripoti kuwa, Kazem Qomi Balozi Mpya na Mjumbe Maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Masuala ya Afghanistan kuhusu jitihada za serikali ya Iran kwa ajili ya kurejesha amani na uthabiti nchini Afghanistan na pia kuzidisha nafasi ya Tehran katika ustawi wa kiuchumii wa nchi hiyo amesema Afghanistan inaweza kutoa mchango katika uchumi wa Iran; na kupanua ushirikiano na nchi hiyo ndio sera ya serikali ya Iran.
Kazem Qomi ameeleza kuwa mapato ya Afghanistan yamepungua kwa zaidi ya asilimia 70; kiasi kwamba tokea Taliban ishike hatamu za kuiongoza nchi iyo, misaada ya jamii ya kimataifa pia imepungua kutoka karibu dola bilioni 13 hadi bilioni 3. Amesema kupungua huko kwa misaada kumeathiri maisha ya wananchi na uchumi wa Afghanistan. Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatambua vyema suala hilo muhimu na hali ya mambo inayoikabili hivi sasa nchi hiyo jirani.
Balozi wa Iran nchini Afghanistan ameongeza kusema kuwa hali ya uchumi wa Afghanistan ni mbaya sana; jambo lililosababisha ongezeko la wimbi la wakimbizi kuelekea katika nchi nyingine khususan Iran; na ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikaliweka katika ajenda yake ya kazi suala la kushirikiana na Afghanistan katika nyanja ya uchumi kama mojawapo ya mikakati yake mikuu pia kwa mtazamo wa kibinadamu, kiakhlaqi na Kiislamu na pia kwa upande wa maslahi.