Kupiga hatua sekta ya mafuta ya Iran licha ya kuandamwa kwa vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i97436-kupiga_hatua_sekta_ya_mafuta_ya_iran_licha_ya_kuandamwa_kwa_vikwazo
Taasisi ya utafiti ya Marekani imetangaza kuwa, takribani kilomita 1900 za mabomba ya mafuta nchini Iran zipo katika hali ya kujengwa na kwamba, licha ya Iran kuandamwa na vikwazo inashika nafasi ya kwanza duniani katika uga huu.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
May 16, 2023 21:56 UTC
  • Kupiga hatua sekta ya mafuta ya Iran licha ya kuandamwa kwa vikwazo

Taasisi ya utafiti ya Marekani imetangaza kuwa, takribani kilomita 1900 za mabomba ya mafuta nchini Iran zipo katika hali ya kujengwa na kwamba, licha ya Iran kuandamwa na vikwazo inashika nafasi ya kwanza duniani katika uga huu.

Mtandao wa Global Energy Monitor umefanya uchunguzi wa miradi ya mafuta katika mataifa mbalimbali duniani na kuandika, takribani nusu ya njia za mabomba ya mafuta zimo katika hali ya kujengwa au mipango yake imeshaandaliwa katika mabara mawili ya Afrika na Asia ambayo zinajumuisha kilomita 4400 za mabomba ya mafuta ambazo ziko katika hali ya kujengwa kwa gharama ya dola bilioni 1404 na kilomita 10,800 za njia ya mabomba ya mafuta ambazo mipango yake imeshaandaliwa na miradi hiyo inatarajiwa kugharimu dola bilioni 59.8.

Taasisi hiyo ya kiutafiti ya Marekani imetoa orodha ya mataifa 20 duniani ambayo yanajenga mabomba ya mafuta yenye urefu mkubwa zaidi ambapo Iran inashikilia nafasi ya kwanza katika faharasa hiyo. Kukiri kushika nafasi ya kwanza duniani Iran katika miradi ya ujenzi wa mabomba ya kusafirisha mafuta kunatokea katika hali ambayo, sekta ya mafuta ya Iran katika muongo mmoja uliopita imeandamwa na vikwazo vikali zaidi. Kuanzia mwaka 2012, Marekani na baadhi ya waitifaki wake wakitumia kisingizio cha miradi ya nyuklia ya Iran ambayo kimsingi inafanyika kwa malengo ya amani iliiwekea vikwazo sekta ya mafuta ya Iran.

Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walikuwa wakifanya njama pia ya kuzuia kuingia hapa nchini vifaa, nyenzo, suhula na bidhaa hitajika na kuikwamisha sekta ya mafuta ya Iran naakuifanya ikabiliwe na matatizo makubwa hasa kwa kutilia maanani kwamba, ilikuwa ikitegemea kudhamini vipuri na vifaa maalumu kutoka nje.

Katika miaka ya hivi karibuni, suala la kuunda vifaa, vipuri na nyenzo zinazohitajika katika sekta ya mafuta, likafanywa kuwa ajenda kuu ya mashirika yanayotengeneza vifaa mbalimbali yakiwemo mashirika ya elimumsingi ya Kiirani. Kwa hima na idili hadi sasa karibu asilimia 85 ya vifaa na bidhaa zimetengenezwa hapa nchini na zilizobakia zimo mbioni kutengenezwa. Kukamilishwa pia miradi ambayo bado haijakamilika ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na ni katika mipango mikuu ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa muktadha huo, kupanuliwa miradi ya ujenzi wa mabomba ya mafuta kunapaswa kutazamwa kama mifano ya wazi katika uga huo.

 

Kuongeza kiwango cha uzalishaji na matokeo yake ni kuuzwa mafuta ya Iran katika masoko ya kimataifa nalo ni katika matunda muhimu ambayo katika miaka hii miwili ya hivi karibuni ni jambo ambalo limechukua kasi. Kwa mfano, uzalishaji wa mafuta ya Iran tangu kuingia madarakani serikali ya awamu ya 13 ya Rais Ibrahim Raisi imepindukia zaidi ya mapipa milioni tatu huku uzalishaji wa gesi ghafi ukiongezeka mno na kufikia maradufu.

Ripoti zinaonyesha kuwa, mwaka jana 2022 Iran iliuza nje ya nchi mapipa milioni 190 zaidi ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake na inatabiriwa kwamba, mwaka huu rekodi hiyo itavunjwa.

Kwa muktadha huo, licha ya vikwazo vyote ilivyowekewa Iran na Marekani pamoja na washirika wake kwa ajili ya kudhoofisha sekta ya mafuta ya Iran na kupunguuza kiwango cha uzalishaji, lakini filihali takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa mno katika uga wa kuuza mafuta na vilevile katika mipango ya ustawi na upanuzi wa sekta ya mafuta. Kutangaza mtandao wa Global Enery Monitor kwamba, Iran inashika nafasi ya kwanza katika uga wa ujenzi wa njia na mabomba ya mafuta ni ushahidi wa wazi unaothibitisha madai haya.