Raisi: Iran iko tayari kuimarisha uhusiano na nchi rafiki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i98396-raisi_iran_iko_tayari_kuimarisha_uhusiano_na_nchi_rafiki
Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuimarisha uhusiano wake na nchi ambazo zimetangaza utayarifu wao wa kuhuisha uhusiano na Tehran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 04, 2023 11:43 UTC
  • Raisi: Iran iko tayari kuimarisha uhusiano na nchi rafiki

Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuimarisha uhusiano wake na nchi ambazo zimetangaza utayarifu wao wa kuhuisha uhusiano na Tehran.

Rais Raisi amesema hayo akihutubia taifa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 34 wa kifo cha muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA)  na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kusimama kidete dhidi ya nchi zinazolihujumu taifa la Iran. 

Amesema mitazamo na fikra za Imam Khomeini (MA) zimetambulika na kupata umaarufu zaidi katika dunia ya leo. Raisi amemtaja  Imam  Ruhullah Khomeini kama kinara wa maendeleo, na kueleza kwamba Kiongozi huyo alikuwa na mtazamo wa kutaka dini itumiwe kama mfumo wa utawala kwa jamii.

Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, misukosuko inayoikumba dunia hii leo imetokana na hatua ya jamii kutenganisha siasa na dini na masuala ya kiroho. Amesema Imam alileta mageuzi makubwa ya kisiasa katika eneo hasasi la Asia Magharibi.

Rais wa Iran amesema mfano hai wa kuonyesha kuwa nidhamu ya dunia imeporomoka, ni dhulma zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina kwa zaidi ya miaka 70 sasa, na pia ukatili wa Marekani na Israel wa kuiangamiza jamii ya wanadamu kwa makombora.

Imam Khomeini (MA)

Raisi amebainisha kuwa, "Nidhamu mpya ya dunia ipo kwa maslahi ya kambi ya muqawama, na Iran itakuwa na nafasi kubwa kwenye nidhamu hiyo."

Amesema alama zote zinaashiria kuwa, ubeberu na uchukuaji maamuzi wa upande mmoja wa Marekani unaporomoka kwa kasi kubwa. Ameongeza kuwa, "Waliodai kuwa na nguvu, hii leo wanakiri juu ya kuongezeka nguvu na ushawishi wa Iran katika eneo.

Raisi ameashiria kauli ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye amekuwa akisisitiza kwamba, chimbuko la uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kasi ya ustawi na maendeleo ya taifa hili licha ya vikwazo.