Msemaji wa Hamas: Ni haki yetu ya msingi kujibu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ametoa mjibizo kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni ya ndege zisizo na rubani katika ngome za muqawama huko Ghaza na kusema kwamba: Mashambulizi hayo hayatasitsiha mapambano ya wanamuqawama wa Palestina dhidi ya utawala huo ghasibu.
Utawala wa Kizayuni jana usiku kwa mara nyingine tena ulishambulia ngome za wanamuqawama wa Palestina huko mashariki mwa Ukanda wa Ghaza. Katika hujuma hiyo, Wazayuni Maghasibu wameshambulia mnara wa ulinzi wa wanamuqawama mashariki mwa Ukanda huo.

Hazem Qassim Msemaji wa Hamas leo Jumanne amesisitiza kuwa, wananchi wa Palestina na muqawama wao wataendelea kuunga mkono mapambano yote ya ukombozi katika medani zote za muqawama kama haki yao ya msingi dhidi ya sera za ukandamizaji na ukaliaji mabavu za utawala wa Kizayuni za kuuyahudisha msikiti wa al Aqsa na jinai zake huko Ukingo wa Magharibi na mzingiro dhidi ya Ghaza.
Kwa siku ya nne mtawalia utawala wa Kizayuni unashambulia maeneo ya wanamuqawama wa Palestina kwa kisingizio kwamba wanamuqawama wanatuma maputo ya moto kuelekea vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Wakati huo huo msemaji wa jeshi la utawala wa Kizayuni amedai kuwa utawala huo umetekeleza mashambulizi ya anga kwa kisingizio kwamba Wapalestina wanatuma maputo ya moto upande wa vitongoji vya walowezi pambizoni mwa Ukanda wa Ghaza.