Feb 29, 2024 12:08 UTC
  • Uthman Taha
    Uthman Taha

Idara ya Haram ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika mji mtakatifu wa Karbala, imetoa heshima maalumu kwa Uthman Taha, kwa kumtangaza mwandishi huyu maarufu wa kaligrafia kama shkhsia bora zaidi wa Qur'ani ya mwaka huu.

Sheikh Uthman Husayn Taha anayejulikana zaidi kwa jina la "Uthman Taha" alikamilisha uandishi wa nakala ya Qur'ani kwa maandishi ya Naskh katika miaka ya 1970, na nakala ya Qur'ani aliyoiandika iliwavutia Waislamu wengi kwa miaka mingi.

Uthman Taha ambaye ni mzaliwa wa Syria amekuwa akiishi katika mji mtakatifu wa Madina kwa miaka kadhaa na ameandika Qur'ani nzima mara kadhaa kwa visomo tofauti.

Kazi ya kushangaza zaidi katika kaligrafia ya nakala ya Qur'ani ya Uthman Taha ni mpangilio maalumu na utaratibu wa aina yake wa kurasa zake kwa kadiri kwamba, mkaligrafia huyo mashuhuri wa Syria amefanikiwa kuweka Aya ndefu zaidi ya Qur'ani Tukufu katika ukurasa mmoja.

Nakala ya Qur'ani iliyoandikwa na Uthman Taha ilisambaa haraka sana katika nchi zote za Kiislamu na kufuta nakala nyingine zilizoandikwa kwa kaligrafia tofauti, na hii leo, baada ya miongo minne ya kuandikwa kwake, bado inatambuliwa kuwa nakala inayotumiwa zaidi ya Qur'ani katika nchi mbalimbali duniani.

Profesa Fadil Salih al-Samarrai, kushoto

Mwaka jana, Idara ya Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali (as) katika mjii wa Karbala ilimchagua Profesa Fadil Salih al-Samarrai kama mtu bora wa mwaka kwa juhudi zake za kielimu katika uwanja wa utafiti wa kisayansi wa Qur'ani Tukufu.