Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-2
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya pili ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Katika kipindi kilichopita tulisema kwamba, ni kwa kutegemea mafundisho ya dini ya Kiislamu yanayosisitiza kwamba viumbe wote wanatokana na irada ya Mwenyezi Mungu, sambamba na kupinga ukandamizaji na dhulma, ndipo Imam Khomeini akasimama na kuongoza jihadi (mapambano) dhidi ya mfumo wa kibeberu uliokuwa unatawala dunia, yaani kambi mbili za Marekani na Urusi ya zamani. Ni katika hali hiyo na kufuatia kuushinda pia mfumo wa ukandamizaji uliokuwa ukitawala nchini Iran, ndipa akawa amepeperusha bendera ya mwamko wa kukabiliana na ubeberu wa dunia kote ulimwenguni. Kadhalika Imam Khomeini kwa kuamini ahadi ya Mwenyezi Mungu kwamba hatimaye wanyonge watawashinda mabeberu, aliwataka watu wote wanyonge kuunda mrengo mmoja jumuishi duniani kwa ajili ya kupeana maarifa, kuanzisha ngome ya muqawama na hatimaye kuunda kambi moja imara kwa ajili ya kupambana na ubeberu wa dunia. Katika uwanja huo, alikuwa akisisitiza kwa kusema: “Nina tumai kwamba jambo hili (la ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) ni utangulizi kwa ajili ya kuundwa (kambi ya mustadhaafina- wanyonge) katika maeneo yote ya dunia ambapo madhaifu wote watashiriki katika kambi hiyo na kuweza kutatua matatizo yote yaliyo mbele yao. Na katika makabiliano dhidi ya mabeberu na kambi za Mashariki na Magharibi waweze kusimama imara na wasiruhusu mabeberu kuwatawala na kuwadhulumu.” Mwisho wa kunukuu.
Wapenzi wasikilizaji ndani ya maktaba ya Imam Khomeini (MA) kulitangazwa rasmi siasa za kutofungamana na “upande wa Mashariki wala wa Magharibi” na ikawa dira ya hatua za utekelezaji za serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika uwanja huo Imam Khomeini alikutaja kutoegemea kambi mbili za Mashariki na Magharibi kuwa njia iliyonyooka ya kisiasa na moja ya sifa za kipekee za Mapinduzi ya Kiislamu na kuhusu hilo alisema: “Mapinduzi ya Kiislamu sio mapinduzi mepesi kama ambavyo hayajaegemea upande wowote wa Mashariki au wa Magharibi, bali mapinduzi haya ya Kiislamu yamesimama dhidi ya kambi hizo mbili.” Mwisho wa kunukuu. Kwa hakika msimamo huo wa Mapinduzi ya Kiislamu umebainishwa wazi katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kipengee cha 10 cha katiba ya Iran ambacho kimeelezea misingi ya siasa za kigeni za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kinasisitiza kupigwa marufuku uhusiano wowote na madola ya kibeberu. Aidha kipengee cha 152 cha katiba hiyo, sambamba na kusisitizia juu ya kujitawala nchi hii na kutofungamana mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na madola ya kibeberu kinasema: “Siasa za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimejengeka juu ya msingi wa kupinga aina yoyote ya kupenda kujitanua au kukubali kutawaliwa, kulinda kujitawala kwa pande zote na ardhi yote ya nchi, kutetea haki za Waislamu, kutofungamana na madola ya kibeberu na kuwa na uhusiano mwema wa pande mbili na madola yasiyokuwa ya kiuadui.” Mwisho wa kunukuu.
***************
Aidha Imam Khomeini (MA) alikutaja kuwaunga mkono wanyonge na wasio jiweza duniani kuwa ni moja ya misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na katika hilo aliamiani kwamba katika kupambana na mabeberu wa dunia, mataifa yenye kudhulumiwa na dhaifu lazima yawe makini na ni lazima mapambano yao dhidi ya mabeberu yaungwe mkono. Imam Khomeini (MA) alisema: “Taifa huru la Iran hadi sasa linaendelea kuyaunga mkono kikamilifu mataifa ya wanyonge duniani katika makabiliano yao na pande ambazo zinatumia mkono wa chuma na mabavu. Tutaziunga mkono harakati zote zinazopigania kujikomboa kote duniani katika njia ya Mwenyezi Mungu na ya haki.” Mwisho wa kunukuu. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kupambana na ubeberu na kuwaunga mkono wanyonge na masikini kunaweza kufikiwa kwa njia ya uelewa wa mataifa sambamba na kufuata mwamko wa wananchi wa Iran na bila ya uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi nyingine. Lengo la mapambano hayo, yawe katika njia ya izza, kupigania uhuru na kujitawala. Suala hilo limeashiriwa pia katika kipengee cha 154 cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kusema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalichukulia suala la saada ya mwanadamu katika jamii nzima ya mwanadamu kuwa lengo lake kuu na kujitawala, uhuru na utawala wa haki na uadilifu kuwa haki ya watu wote duniani. Katika hali hiyo na kwa kujiepusha kikamilifu na aina yoyote ya uingiliaji katika masuala ya ndani ya mataifa mengine, taifa la Iran linaunga mkono mapambano ya haki ya wanyonge dhidi ya mabeberu katika pembe zote za dunia.” Mwisho wakunukuu.
**************
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu pili ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia kiini na kichochezi cha Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya usimamizi wa Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika kubainisha sababu ya kuundwa madola yenye kupenda kujitanua duniani Imam Khomeini (MA) anabainisha mambo matatu. Kwanza ni majigambo ya mabeberu hao. Kwa mtazamo wa Imamu Khomein, chanzo cha ufisadi wote duniani kinatokana na ugonjwa wa kujiona na kujigamba, kwa kuwa suala hilo huibua hisia ya kupenda madaraka na kuwatawala wengine. Pili ni kwa wanyonge wenyewe kujishinda kwa kujiona kuwa hawana uwezo wa kufanya lolote na jambo hilo kuchochewa zaidi na mabeberu wanaolenga kuwakandamiza. Katika kubainisha sababu ya tatu, Imam Khomeini (MA) anaashiria sifa mbili hizo za kuhisi unyonge mataifa ya ulimwengu wa tatu na uistikbari wa madola ya Magharibi katika kuzidhoofisha nafsi za viongozi wa nchi za wanyonge. Kuhusiana na hilo anaamini kwamba, kudhoofisha na kuwatia khofu viongozi wa nchi za wanyonge kunakofanywa na madola ya kibeberu ni miongoni mwa njia muhimu ambazo zimekuwa zikitumiwa na madola hayo kuyakandamiza mataifa ya wanyonge. Hii ni kwa kuwa kwa kuwatia khofu viongozi wa nchi hizo kuhusiana na nguvu bandia za madola hayo na vilevile taamaa yao kubwa ya kuendelea kuyatawala mataifa ya wanyonge huwapokonya viongozi hao ujasiri wa kujaribu kupambana na madola hayo ya kibeberu. Matokeo yake ni kwamba, viongozi hao wenye nafsi dhaifu, hugeuka na kuwa kizuizi na wasambaratishaji wakubwa wa moyo wa hamasa ya watu wa mataifa yao wenyewe katika kupambana na ubeberu na mwamko wa raia wao katika kupigania uhuru wa kujitawala na kukabiliana na dhulma nchini kwao.
*********
Ndugu wasikilizaji ufafanuzi wa ubeberu uliotolewa na Imam Khomeini (MA) umebaki ukiendelezwa na kiongozi wa baada yake, yaani Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambapo naye mara kwa mara na katika matukio tofauti, amekuwa akibainisha misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na ubeberu na kinara wa ubeberu wa dunia yaani Marekani. Kuhusu suala hilo, Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema: “Mfumo wa ubeberu ni nukta inayopingana na mfumo wa Kiislamu. Sisi tunapinga ubeberu na tunapingana nao.” Mwisho wa kunukuu.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya pili ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.