Wabahrain waandamana kuwaunga mkono wafungwa waliogoma kula
(last modified Sat, 19 Aug 2023 10:20:38 GMT )
Aug 19, 2023 10:20 UTC
  • Wabahrain waandamana kuwaunga mkono wafungwa waliogoma kula

Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mjuu Manama, kwa shabaha ya kuwaunga mkono na kusimama pamoja na wafungwa waliogoma kula wakilalamikia hali mbaya ya jela.

Mbali na Manama, maandamano hayo yameshuhudiwa pia katika miji ya kaskazini ya Jidhafs na al-Maqsha, na vile vile katika vitongoji vya Sanabis na al-Daih.

Waandamanaji hao wamelaani dhulma na ukandamizaji wanaofanyiwa wanaharakati wa kisiasa wanaozuiliwa katika jela na magereza mbalimbali ya nchi hiyo ya Kiarabu, hasa katika gereza 'sugu' la Jau.

Huku wakiwa wamebeba picha za mwanachuoni mkubwa wa Kishia nchini humo, Ayatullah Sheikh Isa Qassim, wananchi hao Bahrain wametaka kuachiwa huru mara moja na bila masharti wafungwa wa itikadi, waliorundukana katika jela na vituo mbalimbali nchini humo.

Kadhalika wamesikika wakipiga nara dhidi ya utawala wa Aal-Khalifa, wakisisitiza kuwa unapasa kubebeshwa dhima ya maisha ya wafungwa hao wa kisiasa.

Ijumaa ya wiki iliyopita, Jumuiya ya al-Wefaq ya Bahrain ilitangaza kwamba, mamia ya wafungwa wa Bahrain wamegoma kula wakilamikia hali ngumu ya magereza ikiwa ni pamoja na kuwekwa ndani ya seli kwa muda wa saa 23 kwa siku na kuzuiwa kufanya shughuli za kidini.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakiilaani  serikali ya Bahrain kwa kuwakandamiza wapinzani na yametoa wito wa kufanyika marekebisho katika mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.