Ijumaa, tarehe 14 Februari, 2025
Ijumaa tarehe 15 Shaaban 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 14 Februari 2025.
Siku kama ya leo miaka 1191 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (as) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra Kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq.
Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa, na al Qaim, kwa maana ya atakayeanzisha mapambano.
Imam Mahdi alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa na baba yake mpendwa, Imam Askari (as). Alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu na kisha akatoweka na kwenda ghaiba kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu na atadhihiri tena ulimwenguni wakati mwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa.
Atakapodhihiri duniani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huadhimishwa nchini Iran kama Siku ya Waliodhulumiwa Duniani.

Miaka 87 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni waliokuwa na silaha na wanachama wa kundi la kigaidi la Palmach waliendeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Palestina kwa kutekeleza shambulizi la kigaidi dhidi ya wakazi wa kijiji cha Sa'sa' huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Katika operesheni hiyo iliyoendelea hadi kesho yake nyumba 20 za raia wa Palestina ziliharibiwa na watu 60 waliokuwemo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo, wakauawa kwa umati.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita sawa na tarehe 14 Februari mwaka 1945, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia nchi mbili za Marekani na Uingereza zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo ya Ujerumani.
Ndege 1773 za kijeshi zilitumiwa katika mashambulizi hayo ambayo ndiyo yaliyokuwa na hasara kubwa zaidi ya mali na nafsi duniani hadi hii leo. Mashambulizi hayo ya kinyama ya Marekani na Uingereza yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tatu yalisawazisha na ardhi miji kadhaa ya viwanda ya Ujerumani na kuifanya majivu matupu.
Raia kati ya laki moja na nusu hadi laki mbili na nusu waliuawa kinyama katika mashambulizi hayo.

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, Martin Scott tabibu mpasuaji wa Uingereza alifanikiwa kuunganisha figo ya mwanadamu.
Siku hiyo Prf. Scott alichukua figo ya mtu aliyekuwa amefariki dunia na kuiunganisha kwa mafanikio na mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika hospitali moja ya Leeds huko Uingereza.****
Katika siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, aliuawa Rafiq Hariri Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon kwenye mlipuko wa bomu lililotegwa garini huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon.
Alikuwa mmoja wa wafanyabiashara tajiri nchini Lebanon na wakati alipofariki dunia alikuwa na umri wa miaka 61.
Hariri alichukua wadhifa wa Uwaziri Mkuu wa Lebanon kutokea mwaka 1992, muda mfupi baada ya kumalizika vita vya ndani vya Lebanon hadi mwaka 1998, na kuchukua tena wadhifa huo mwaka 2000 hadi 2004.
