OIC: Papua New Guinea imefanya makosa kwa kufungua ubalozi Quds
(last modified Fri, 08 Sep 2023 07:37:48 GMT )
Sep 08, 2023 07:37 UTC
  • OIC: Papua New Guinea imefanya makosa kwa kufungua ubalozi Quds

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imekosoa vikali hatua ya Papua New Guinea kufungua ubalozi katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

OIC imesema hatua ya nchi hiyo kufungua ubalozi katika mji mtukufu wa Quds ni batili na inakiuka sheria za kimataifa pamoja na maazimio ya Umoja wa Mataifa, hasa Azimio Nambari  478 (1980) la Baraza la Usalama la UN.

Jumanne wiki hii, Papua New Guinea ilifungua ubalozi wake mjini Quds, na kuwa nchi ya tano kufungua ofisi ya kidiplomasia katika mji huo mtukufu unokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu.

Ikumbukwe kuwa, Disemba mwaka 2017 aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuwa Washington inaitambua Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel na kisha kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel Aviv. 

Baadhi ya nchi kama Honduras, Kosovo, Guatemala na Paraguay zimefuata kibubusa sera za Washington na kuafiki suala la kuhamisha balozi zao kutoka Tel Aviv kwenda mji wa Quds, kitendo ambacho kinakiuka sheria za kimataifa. Hata hivyo Paraguay ilifutilia mbali uamuzi huo miezi minne baadaye.

OIC imeitaka Papua New Guinea iangalie upya uamuzi wake huo, ikisisitiza kuwa jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuongeza jitihada za kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Palestina-Israel kwa msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.