Bashar Assad: Marekani inashirikiana na magaidi
(last modified Sat, 30 Sep 2023 07:16:46 GMT )
Sep 30, 2023 07:16 UTC
  • Bashar Assad: Marekani inashirikiana na magaidi

Rais Bashar al-Assad wa Syria amezungumzia kuwepo kwa magaidi katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na jinsi Marekani ilivyo na udhibiti kamili wa maeneo hayo na kusisitiza kwamba Washington inashirikiana na magaidi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Rais Bashar al-Assad wa Syria ameeleza hayo katika  mahojiano na televisheni ya China CCTV na kubainisha kuwa, "vita havijaisha na kwa sasa tuko katikati ya mapambano. Lakini Syria daima imekuwa ikikabiliawa na hujuma kwa nafasi yake ya kijiografia. Hata hivyo, watu wa Syria wataweza kuijenga upya nchi yao pindi vita vitakapomalizika na kuondolewa mzingiro".

Askari vamizi wa jeshi la kigaidi la Marekani wakiwa ndani ya ardhi ya Syria

Bashar Assad ameongeza kuwa: eneo la kaskazini mashariki mwa Syria, ambalo magaidi wanalikalia, liko mahali ambako Marekani ina udhibiti kamili. Kwa hiyo, suala si la wizi tu unaofanywa na Marekani kwa rasilimali za taifa la Syria, bali pia ni ushirikiano wake na magaidi katika kugawana faida. Wakati huo huo inasababisha pia tatizo la pili ambalo ni kwa nchi hii kubwa duniani kushirikiana na magaidi.

Assad ameashiria tatizo la hali ya maisha ya wananchi wa Syria inayotokana na hali mbaya ya kiuchumi, na kueleza kwamba: Iwapo itajengwa upya, Syria ijayo itakuwa na mustakabali mzuri mno. Kabla ya vita, uchumi  wa Syria ulikuwa unakua kwa kiwango bora cha 7%, ambayo ilionekana kuwa ni kiwango cha juu sana kwa nchi yenye uwezo mdogo. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwa uhakika kamili kwamba kusimamishwa vita na kujengwa upya nchi kutaifanya Syria iwe bora zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa kabla ya vita.../

Tags