Hamas yasema Marekani inawasaidia Wazayuni katika vita vya Ghaza
(last modified Thu, 02 Nov 2023 06:19:24 GMT )
Nov 02, 2023 06:19 UTC
  • Hamas yasema Marekani inawasaidia Wazayuni katika vita vya Ghaza

Mmoja wa viongozi wa kundi la Wanamapambano wa Kiislamu wa Palestina Hamas amesema Marekani inaunga mkono na kuusaidia kwa hali na mali Utawala wa Kizayuni katika mapigano ya Ghaza.

Kwa mujibu wa tovuti ya al-Masira, Ali Baraka, mmoja wa viongozi wa harakati ya Hamas nje ya nchi, amesema Watu wa Palestina wanauawa kinyama na mabomu ya kisasa ya Marekani.

Barkeh ameongeza kuwa: Tumeingia katika kipindi cha muqawama ambapo utawala wa Kizayuni unaelekea kutokomea na kuangamia na nchi zinazofanya mapatano nautawala huo zinapaswa kuangalia upya sera zao.

Mwanachama huyo wa Hamas amesisitiza kwamba wanamapambano wanatetea na kuulinda Msikiti wa Al-Aqsa pamoja na heshima ya Umma wa Kiarabu.

Huku akiwapongeza wanajeshi wa Yemen ambao wanatoa uungaji mkono kwa wanamuqawama wa Palestina, Baraka ameongeza kwamba wakati makombora na ndege zisizo na rubani zinaporushwa kutoka Yemen, zina ujumbe kwamba Yemen kamwe haitaliacha pekee taifa la Palestina.

Kiongozi huyo wa harakati ya Hamas aidha amesisitiza kuwa, adui Mzayuni anaelewa tu lugha ya nguvu na operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa imefungua mlango wa kukombolewa ardhi ya Palestina, na kufunga mwanya wa uwezekano wa kuimarishwa sera na siasa mbovu na za kighasibu za utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Ali Barka amesema: Taathira za operesheni ya Kimbunga cha  Al-Aqsa hazitaishia tu katika Ukanda wa Ghaza, bali zitaenea katika nchi zote.

Wizara ya Afya ya Ukanda wa Ghaza imetangaza kwamba, idadi ya mashahidi  imeongezeka na kufikia 8,796 tangu kuanza kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda huo tarehe 7 Oktoba.

Tags