Wazayuni waendeleza jinai Ghaza, waliouawa shahidi wakaribia 15,000
Ofisi ya Upashaji Habari ya Serikali ya Palestina huko Ghaza, usiku wa kuamkia leo Jumatano imetangaza kuwa, idadi ya wananchi wa Palestina waliouawa shahidi kwenye mashambulizi ya kikatili ya Israel imekaribia 15,000.
Ofisi hiyo imesema kuwa, idadi ya wahanga hao inaongezeka kila sekunde na hadi wakati wanatangaza habari hiyo, wananchi 14,128 wa Palestina walikuwa wameshathibitishwa kuuawa shahidi, 6,000 kati yao ni watoto wadogo na 3,920 ni wanawake.
Taarifa ya ofisi hiyo imeongeza kuwa, zaidi ya Wapalestina 6,800 hawajapatikana na hawajulikani walipo, lakini wengi wao wako kwenye vifusi vya majengo yaliyobomolewa kwa chuki na uadui na wanajeshi madhalimu wa Israel.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, idadi ya wananchi wa Palestina waliokuwa wamejeruhiwa hadi jana usiku ilikuwa imepindukia 33,000 ambapo zaidi ya asilimia 75 kati yao ni wanawake na watoto wadogo.
Taarifa ya ofisi hiyo ya Upashaji Habari ya Serikali ya Palestina huko Ghaza imeongeza kuwa, nyumba 44,000 zimevunjwa kikamilifu na laki mbili na 30,000 zimesababishiwa hasara na mashambulio ya kinyama ya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza uliozingiwa kila upande kwa miaka mingi. Zaidi ya asilimia 60 ya nyumba za eneo la Ghaza zimepata uharibifu kutokana na jinai hizo za Wazayuni.
Jumamosi ya tarehe 7 Oktoba, 2023 imerekodiwa katika orodhha ya siku muhimu mno kwenye historia ya mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Siku hiyo wanamapambano wa Palestina wakiongozwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya HAMAS waliendesha operesheni ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa na kutoa pigo kubwa la kihistoria dhidi ya mfumo wa kijeshi, kiusalama, kiuchumi na kiintelijensia wa utawala pandikizi wa Israel.
Baada ya kushindwa na kupata pigo kwenye medani ya vita, utawala wa Kizayuni umeamua kumalizia hamaki zake kupitia kuua watoto wachanga, watoto wadogo, wanawake na vizee na kuharibu makazi ya raia, Misikiti, makanisa, mahospitali, maskuli na miundombinu ya Ukanda wa Ghaza.