Kiongozi wa Hizbullah akutana na maafisa waandamizi wa HAMAS Beirut
Katibu Mkuu wa Hizbullah jana Jumatano alikutana na ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS mjini Beirut kujadili matukio ya Gaza, huku idadi ya wananchi wa Palestina waliouawa shahidi kwenye mashambulizi ya kikatili ya Israel katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu ikikaribia 15,000.
Kwa mujibu wa televisheni ya al-Mayadeen inayotangaza kwa lugha ya Kiarabu, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah alikutana na maafisa wa ngazi za juu wa HAMAS, wakiwemo Khalil al-Hayya na Osama Hamdan mapema jana katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Katika mkutano huo, Sayyid Nasrullah na maafisa wa HAMAS walijadili matukio ya hivi karibuni katika eneo kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, operesheni kubwa zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina dhidi ya utawala huo ghasibu.
Pande mbili hizo zimesisitizia haja ya makundi ya muqawama kuwa na ushirikiano wa karibu na kusimama kidete ili muqawama uibuke mshindi mkabala wa adui Mzayuni.
Mkutano huo umefanyika siku moja baada ya wanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon kuanzisha wimbi la mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za utawala wa Kizayuni kaskazini mwa nchi.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya al-Manar, Hizbullah juzi Jumanne ilishambulia kituo cha kijeshi cha Wazayuni cha al-Raheb kwa kutumia kombora la Burkan.
Aidha wanamuqawama wa Hizbullah wameshambulia maeneo ya Bayyad Blida na Yiftah yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.