Mchambuzi Mzayuni: HAMAS wamejipanga vizuri kwa vita, tofauti na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105158-mchambuzi_mzayuni_hamas_wamejipanga_vizuri_kwa_vita_tofauti_na_israel
Mchambuzi mmoja Mzayuni amesema kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imejipanga vizuri na inaendesha kwa umahiri wa hali ya juu vita vya Ghaza, tofauti na Israel ambayo malengo yake hasa, hayajulikani na haifahamiki inaendesha vita vya Ghaza kwa mikakati gani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 23, 2023 23:21 UTC
  • Mchambuzi Mzayuni: HAMAS wamejipanga vizuri kwa vita, tofauti na Israel

Mchambuzi mmoja Mzayuni amesema kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imejipanga vizuri na inaendesha kwa umahiri wa hali ya juu vita vya Ghaza, tofauti na Israel ambayo malengo yake hasa, hayajulikani na haifahamiki inaendesha vita vya Ghaza kwa mikakati gani.

Hayo yameripotiwa na gazeti la Kizayuni la Maariv ambalo limezungumzia makubaliano ya kusimamisha vita kwa muda wa siku nne kati ya utawala wa Kizayuni na wanamapambano wa Palestina huko Ghaza na kukiri kuwa, HAMAS na kamanda wake Yahya Sinwar, wanakwenda kwa mkakati maalumu na hatua kwa hatua kwenye vita kiasi kwamba hata wamepanga namna ya kutoka na ushindi kwenye vita hivyo na kila ratiba yao wamejiwekea ratiba mbadala, ikifeli hii watumie hii, lakini Israel haionekani kuwa na stratijia maalumu katika vita hivyo.

Mchambuzi huyo maarufu, Moshe Elad ameandika katika makala yake hiyo kwenye toleo la Jumatano la gazeti la Kizayuni la Maariv kwamba, kamanda wa HAMAS, Yahya Sinwar anaujua vizuri sana udhaifu wa Waisraili.

Viongozi wa makundi ya muqawama Palestina wanapendwa sana na wananchi. Yahya Sinwar akiwa katikati ya kundi la watu.

 

Katika sehemu nyingine ya makala yake hiyo, mwandishi huyo Mzayuni, Moshe Elad amesema, hivi sasa kiongozi wa HAMAS Yahya Sinwar amefanikiwa kuilazimisha Israel isimamishe vita na ikubali kuwaachilia huru Wapalestina 150 mkabala wa kuachiliwa huru mateka 50 tu wa Kizayuni. Amesema: HAMAS watatumia kipindi hiki cha kusimamishwa vita kujipanga upya na kurekebisha kila penye makosa huku wakiwa wamefanikiwa kuwaachilia huru idadi kubwa ya Wapalestina walioko kwenye jela za Israel. Vile vile amesema: HAMAS watapata fursa pia ya kuingiza chakula na madawa ndani ya Ukanda wa Ghaza na hayo yote ni mafanikio kwa Wapalestina na ni pigo kwa Israel.

Kitu kingine ambacho mwandishi huyo Mzayuni amekiri ni kwamba msamiati wa kujisalimisha haumo kwenye kamusi ya wanamapambano wa Palestina akiwemo kamanda wa HAMAS, Yahya Sinwar.