Hali si hali kwa wanajeshi wa Israel Ghaza, wakimbia, waadhibiwa
Duru za habari za Kizayuni zimefichua kuwa, hali si hali kwa wanajeshi wa Israel katika vita vya Ghaza kiasi kwamba jeshi la utawala wa Kizayuni limelazimika kuweka adhabu kali sana kutokana na kuongezeka idadi ya wanajeshi wa Israel wanaokimbia vitani kwa woga na kiwewe kilichowapata.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, duru za habari za Kizayuni zimetangaza kuwa, kabla ya Israel kuanzisha vita vikubwa dhidi ya Wapalestina huko Ghaza, iliweka sheria kali sana kwa wanajeshi wa Israel wanaokimbia vitani kwani ilijua kuwa vita hivyo si lele mama.
Duru hizo za habari za Israel zimeongeza kuwa, baada ya kupita karibu miezi miwili tangu kuanza vita vya Ghaza, utawala wa Kizayuni umelazimika kuweka adhabu kali zaidi kwa wanajeshi wanaokimbia kwenye medani za vita.
Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya Kizayuni, hivi sasa wanajeshi 2000 wa Israel wamekimbia jeshini. Baadhi yao walikimbia kabla ya vita vya hivi sasa vya Ghaza vilivyoanza tarehe 7 Oktoba. Mamia ya wanajeshi wengine wa akiba wa Israel wanakwepa kujiunga kwenye operesheni za nchi kavu za Ghaza.
Huku hayo yakiripotiwa, mwanajeshi mmoja wa Israel aliyeko kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ameiambia kanali ya 12 ya televisheni ya Israel kwamba kambi zao zina upungufu mkubwa wa chakula na zana za kivita. Amelalamika pia kulala kwenye magari ya wagonjwa katika kipindi hiki cha baridi kali na hakuna misaada yoyote ya fedha na vifaa wanavyopatiwa na serikali na Benjamin Netanyahu.
Kanali hiyo ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imetangaza pia kuwa, siku chache tu baada ya kuanza vita vya hivi sasa vya Ghaza, jeshi la anga la Israel liliwaita Israel mamia ya wanajeshi wa kawaida na wa akiba kutoka kona zote za Ulaya suala ambalo limeusababishia utawala wa Kizayuni hasara kubwa za kiuchumi na zana za kijeshi.