Usitishaji vita wa muda Gaza waanza kutekelezwa
Usitishaji vita wa siku 4 huko Ukanda Gaza umetekelezwa katika siku ya 49 ya vita kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni.
Usitishaji huu wa mapigano ulipaswa kutekelezwa jana (Alhamisi) saa 10 kamili kwa saa za huko Gaza, lakini kutokana na masuala ya kiufundi na ya usaidizi yaliotajwa, umetekelezwa kuanzia leo huko Gaza kwa kucheleweshwa kwa siku moja.
Ripoti ya shirika la habari la Tasnim imeongeza kuwa, kwa mujibu wa usitishaji vita huo wa siku 4, hatua zozote za kijeshi kati ya Hamas na vikosi vya Kizayuni zitasitishwa katika siku za usitishaji vita. Aidha inatazamiwa kuwa wanawake 4 na mtoto wa Kipalestina waliokuwa katika jela za utawala wa Kizayuni wataachiwa huru mkabala wa kila mfungwa mmoja wa Kizayuni. Wakati huo huo mateka 50 wa Israel wataachiwa huru katika muda huu wa siku nne za usitishaji vita wa muda.
Aidha malori 200 yenye bidhaa za chakula na vifaa vya matibabu yataelekea katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza huku malori manne ya mafuta na gesi ya kupikia yatatumwa Ukanda wa Gaza kila siku.
Inafaa kuashiria hapa kuwa leo ssubuhi ya leo saa moja kabla ya kutekelezwa usitishaji vita wa muda huko Gaza, utawala wa Kizayuni ulishadidisha mashambulizi yake ya anga na mizinga katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza hususan kaskazini mwa eneo hilo.
Ripoti zinasema kuwa watu kadhaa wakiwemo baadhi ya watoto wameuawa shahidi katika shambulio la bomu lililotekelezwa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika nyumba moja ya raia kwenye kambi ya Al-Nusirat huko katikati mwa Ukanda wa Gaza.