Kukaribishwa kwa shangwe wafungwa walioachiwa huru huko Palestina
Idadi kubwa ya wananchi wa Palestina wamewakaribisha kwa furaha kubwa wafungwa walioachiliwa huru wa Kipalestina kutoka jela za utawala wa Kizayuni kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa IRNA; Kitongoji cha Bitonya kimekuwa moja ya maeneo ambayo idadi kubwa ya watu imewapokea kwa shangwe wanawake na watoto walioachiliwa huru kutoka katika jela za utawala wa Kizayuni.
Idara ya Wafungwa wa Palestina imethibitisha usiku wa kuamkia leo kwamba jeshi la Kizayuni limewachia huru wafungwa hao ambao ni wanawake 24 na watoto 15.
Taarifa ya idara hiyo imetangaza kwamba kundi hilo ni la kwanza kuachiliwa huru kwa kuzingatia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Usitishaji vita wa siku nne kati ya utawala wa Kizayuni na harakati ya muqawama ya Palestina Hamas ulianza Ijumaa ya jana saa moja asubuhi.
Wanamuqawama wa Palestina walianzisha operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni tarehe 7 Oktoba ikiwa ni katika kukabiliana na zaidi ya miongo saba ya uvamizi wa utawala huo dhidi ya watu wa Gaza na maeneo mengine ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Kama kawaida, utawala wa Kizayuni umekuwa ukishambulia kwa mabomu maeneo ya raia na kuwaua kwa umati raia wasiokuwa na hatia ikiwa ni katika kujibu hatua hiyo ya kishujaa ya wanamapambano wa Kipalestina.
Hatimaye, utawala huo umekubali kushindwa katika operesheni yake ya kuwakomboa mateka na kusalimu amri mbele ya matakwa ya Wapalestina.