Jihad al Islami: Tumewaandalia Wazayuni majibu wanayostahiki kama watavunja makubaliano
Msemaji wa Brigedi za Quds, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina ameuonya utawala wa Kizayuni kuwa umeandaliwa majibu unayostahiki kama hautoheshimu mapatano ya kusimamisha vita huko Ghaza.
Abu Hamza amesema katika ujumbe wake huo wa sauti kwamba: Sisi tumetangaza kuwa tutaheshimu makubaliano ya kusimamisha vita kwa muda uliopanga lakini kwa sharti kwamba adui naye aheshimu makubaliano hayo na iwapo atayavunja basi tumemuandalia majibu makali anayostahiki.
Msemaji huyo wa tawi la kijeshi la Jihad al Islami alisema hayo jana Ijumaa mara baada ya kuanza kutekelezwa mapatano ya kusimamisha vita kwa muda wa siku nne baina ya utawala wa Kizayuni na wanamapambano wa Palestina huko Ghaza.
Ameongeza kuwa, Hizbullah ya Lebanon nayo imetoa pigo kubwa kwa adui kama ambavyo pia muqawama wa Iraq umetoa pigo kubwa kwa kambi za kijeshi za Marekani bila ya kusahau kazi kubwa waliyoifanya wanamapambano wa Yemen ambao kwa kuteka kwao meli ya Israel kwenye Bahari ya Sham, wamemfahamisha adui kuwa, Wazayuni hawana haki ya kisheria ya kutumia Bahari Nyekundu.
Wakati huo huo mkuu wa ofisi ya HAMAS ya Mashahidi, Mateka na Majeruhi wa Palestina amesema kuwa, ushujaa wa kupigiwa mfano wa wanamaapambano wa Palestina ndio uliomlazimisha adui Mzayuni kukubali kusimamisha vita kwa masharti yaliyowekwa na Wapalestina.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Zahir Jabbarin akisema hayo usiku wa kuamkia leo Jumamosi baada ya Israel kuwaachilia huru mateka 39 wa Palestina ambao ni wanawake na watoto na kuongeza kuwa, kusimama imara taifa lenye subra na ushujaa la Palestina huko Ghaza, kumesambaratisha njama za Wazayuni za kutaka kuwahamisha kutoka kwenye ardhi zao.