Kuhani wa Kiyahudi asema: Netanyahu ni kafiri
Nov 28, 2023 09:47 UTC
Kuhani mmoja wa Kiyahudi ameeleza bayana kuwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ni kafiri na akasisitiza kwamba kwa mujibu wa Taurati, ni haramu kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina.
Chaim Sofer, kiongozi wa harakati ya Uyahudi wa Othodoksi ya Neturei Karta ameyasema hayo katika mahojiano na chaneli ya televisheni ya Russial-Yaum, ambapo sambamba na kuashiria kwamba mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Gaza ni mauaji na jinai amesisitiza kuwa, nchi za dunia zinapaswa kuzuia uendelezaji wa jinai hizo.
Kiongozi huyo wa Kiyahudi wa madhehebu ya Othodoksi amesisitiza kwa kusema: "tunalaani mauaji ya Gaza, ambayo hadi sasa yamepelekea maelfu ya watu, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto kupoteza maisha yao. Nchi za ulimwengu, hususan Russia na Marekani zinapaswa kutuma jeshi la kimataifa la kwenda kulinda haki za raia wa Palestina na kuzuia kuendelea kwa mauaji haya".
Kiongozi wa harakati ya Uyahudi wa Othodoksi ya Neturei Karta ameongeza kuwa, "tunakaribisha usitishaji vita, lakini inasikitisha kuona usitishaji vita huu ni wa muda tu na tumesikia vitisho vipya kutoka kwa Wazayuni kwamba wataiangamiza Gaza. Tunatumai kushuhudia huko Gaza ujenzi mpya wa nyumba za Wapalestina zilizobomolewa na wanajeshi wa Kizayuni".
Katika kumbukumbu ya Siku ya Nakba, Wayahudi wa harakati ya Neturei Karta huwa wanachoma moto bendera ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel huko Quds Tukufu (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu.../