Usitishaji vita huko Gaza warefushwa kwa siku moja
Asubuhi ya leo Alhamisi , Qatar imetangaza kurefushwa kwa siku moja usitishaji vita kati ya utawala wa Kizayuni na muqawama wa Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Isna, Majid Al-Ansari, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Qatar ametangaza kuwa, pande za Palestina na Israel zimekubaliana kurefusha usitishaji vita kwa siku nyingine moja.
Harakati ya Hamas pia imethibitisha kurefushwa usitishaji vita kwa siku nyingine moja. Kuhusiana na hilo jeshi la Kizayuni pia limetangaza kuwa, litaendeleza usitishaji vita wa kibinadamu ili kuruhusu kuachiliwa huru mateka zaidi wa Kizayuni.

Jumatano iliyopita na baada ya siku kadhaa za mazungumzo yasiyokuwa ya moja kwa moja, utawala wa Kizayuni na muqawama wa Palestina zilifikia makubaliano ya usitishaji vita wa siku nne na kubadilishana mateka.
Kwa mujibu wa makubaliano ya kubadilishana mateka ambayo awamu yake ya kwanza ilianza kutekelezwa Ijumaa, ili kuachiliwa huru mzayuni mmoja, wafungwa watatu wa Kipalestina itabidi waachiliwe kutoka jela za utawala wa Kizayuni. Makubaliano hayo yalifikiwa huku utawala wa Kizayuni ukilazimika kukubali masharti ya makundi ya wanamapambano wa Kipalestina katika uwanja huo. Usitishaji mapigano huo ulirefushwa muda kwa siku mbili zaidi siku ya Jumatatu.