Kuanza tena kesi ya Netanyahu kuhusu tuhuma za ufisadi.
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105582-kuanza_tena_kesi_ya_netanyahu_kuhusu_tuhuma_za_ufisadi.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa kikao cha kufuatilia kesi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo kitafanyika leo Jumatatu.
(last modified 2023-12-04T02:40:16+00:00 )
Dec 04, 2023 02:40 UTC
  • Kuanza tena kesi ya Netanyahu kuhusu tuhuma za ufisadi.

Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa kikao cha kufuatilia kesi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo kitafanyika leo Jumatatu.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Sama la Palestina, gazeti la Israel la Kiebrania la Hayom limetangaza kuwa kesi ya Netanyahu kuhusiana na tuhuma za ufisadi itaanza kusikilizwa leo Jumatatu, licha ya kuendelea vita huko Gaza.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kizayuni, mahakama ya utawala wa Kizayuni itaanza kushughulikia kesi za kashfa na tuhuma za ufisadi zinazomkabili Benjamin Netanyhu waziri mkuu wa utawala huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo vikao vya mahakama vya kusikiliza kesi zinazomkabili waziri mkuu huyo vilisimamishwa mwezi Septemba.

Waziri mkuu wa Kizayuni

Katika vikao vya kesi ya Netanyahu zinazohusu tuhuma za rushwa, ushahidi wa maafisa wa polisi wa utawala wa Israel na afisa wa fedha utasikilizwa katika mojawapo ya kesi tatu za mashtaka yao, inayojulikana katika vyombo vya habari kwa jina la "kesi 4000".

Kwa mujibu wa ripoti ya kanali ya 12 ya televisheni ya Kizayuni, kesi ya Netanyahu  hivi sasa iko katika hatua ya mashahidi wa upande wa mashtaka, na baada ya hapo  ni Netanyahu mwenyewe atatoa ushahidi.

Ingawa mchakato huo utachukua muda mrefu, lakini kuanzishwa tena kesi hiyo kutakuwa na athari mbaya kwa waziri mkuu huyo katili mbele ya fikra za waliowengi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) katika mazingira ya hivi sasa ya vita dhidi ya Gaza. Waziri Mkuu huyo anakosolewa na pande zote za Wazayuni kwa kufanya uzembe na kushindwa kukabiliana na Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyoanzishwa na wanamapambano Wapalestina tarehe 7 Oktoba.

Netanyahu anakabiliwa na tuhuma tatu za ufisadi na kupokea hongo, tuhuma ambazo anajaribu kuzikwepa.

Kuhusiana na suala hilo, mwezi Machi mwaka jana, baraza la mawaziri la Netanyahu kupitia waungaji mkono wake bungeni lilipitisha sheria ambayo inabainisha mazingira ambayo waziri mkuu anafaa kuondolewa madarakani.

Madhumuni ya sheria hiyo ni kuzuia kuondolewa madarakani waziri mkuu, isipokuwa katika kesi zinazohusiana na afya yake ambazo zinamzuia kuendelea na kazi. 

Sheria hii pia inajumuisha vipengee vingine kama vile kupigiwa kura na theluthi mbili ya wajumbe wa baraza la mawaziri, pamoja na wajumbe 80 kati ya wabunge 120 wa bunge la Israel.

Tarehe 7 Oktoba, Mahakama ya Juu ya utawala wa Kizayuni ilichunguza uwezekano wa kufuta sheria hiyo.