Yemen yaonya kuzishambulia meli zinazoelekea upande wa utawala wa Kizayuni
Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimetoa taarifa vikitadharisha kuwa vitazuia meli zote zinazoelekea Israel bila kujali ni za nchi gani iwapo Gaza haitapata misaada ya chakula na dawa za matibabu.
Taarifa hii ilitolewa jana usiku na Msemaji wa jeshi la Yemen Brigedia Jenerali, Yahya Saree. "Iwapo Ukanda wa Gaza hautapatiwa misaada ya chakula na dawa za matibabu; vikosi vyetu vya ulinzi vitazishambulia meli zote zilizoko katika bahari Nyekundu kuelekea katika bandari za utawala wa Kizayuni wa Israel,' amesema Brigedia Jenerali Yahya Saree.
Jeshi la Yemen limeyaonya makampuni yote ya usafirishaji baharini kuhusu kushirikiana na utawala wa Israel likisema kuwa mafuruku hiyo inafuatia oparesheni zilizofanikiwa za Yemen za kuzizuia meli za Israel kupita katika bahari za Kiarabu na Nyekundu.
Tangu vita vya Gaza vianze Oktoba 7 mwaka huu jeshi la Yemen limeanzisha oparesheni mtawalia dhidi ya meli zenye mfungamano na utawala wa Kizayuni katika bahari Nyekundu na kutekeleza mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya ngome na maeneo mbalimbali ya Israel katika kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina waliozingirwa huko Gaza.