Mashambulizi makubwa ya utawala wa Kizayuni katikati mwa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105822-mashambulizi_makubwa_ya_utawala_wa_kizayuni_katikati_mwa_gaza
Utawala wa Kizayuni umeendelea kuwashambulia raia na kulenga makazi yao huko Ukanda wa Gaza katika siku ya 65 tangu kutekelezwa oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa.
(last modified 2026-06-17T03:32:54+00:00 )
Dec 10, 2023 03:29 UTC
  • Mashambulizi makubwa ya utawala wa Kizayuni katikati mwa Gaza

Utawala wa Kizayuni umeendelea kuwashambulia raia na kulenga makazi yao huko Ukanda wa Gaza katika siku ya 65 tangu kutekelezwa oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa.

Makundi ya muqawama ya Palestina Oktoba 7 mwaka huu yalitekeleza oparesheni ya aina yake ya kushtukiza kwa jina la Kimbunga cha Al Aqsa dhidi ya ngome za utawala wa Israel; ambapo baada ya kupita siku 45 za vita; pande mbili za Israel na Hamas zilitekeleza mapatano ya kusimamisha vita kwa muda wa siku 4 kwa lengo la kubadilishana mateka wa Israel na Palestina. 

Usitishaji vita huo ulirefushwa muda kwa mara nyingine tena kwa siku mbili na kisha kwa siku nyingine moja; na hatimaye Ijumaa tarehe Mosi Disemba usitishaji vita huo wa muda ulimalizika na utawala wa Kizayuni ukaanzisha tena mashambulizi dhidi ya Gaza.  

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni leo asubuhi umezishambulia kambi za al Bureij, al Maghazi na Deir al Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza. Utawala wa Kizayuni umeshambulia eneo moja la makazi ya raia katika kambi ya al Bureij katikati mwa Gaza na kuwauwa shahidi Wapalestina wasiopungua saba na kujeruhi wengine wengi. 

Mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katikati ya Gaza 

Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni pia zimeshambulia makazi ya raia katika kambi ya al Nusairat katikati ya Gaza na kuwauwa shahidi Wapalestina watatu na kujeruhi wengine kadhaa.