HAMAS: Hatutawaachia mateka wa Israel mpaka matakwa yetu yatakapotekelezwa
(last modified Mon, 11 Dec 2023 03:48:14 GMT )
Dec 11, 2023 03:48 UTC
  • HAMAS: Hatutawaachia mateka wa Israel mpaka matakwa yetu yatakapotekelezwa

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema, kamwe haitasalimu amri kwa mashambulizi ya kinyama ya mtawalia yanayofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza ili iwaachilie mateka wa utawala huo iliowakamata katika operesheni yake ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekeleza mapema mwezi Oktoba.

Msemaji wa tawi la kijeshi la Hamas la Izzuddin al-Qassam anayejulikana kwa lakabu ya Abu Obeida amesema katika taarifa aliyotoa jana Jumapili kuwa njia pekee ya kundi hilo kuwaachilia huru mateka wa Israel wakiwa hai ni kwa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake kukubali masharti ya Hamas likiwemo la kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni.

Abu Obeida ameeleza bayana kuwa: "si adui wa kifashisti na uongozi wake wenye kiburi... wala waungaji mkono wake... wanaweza kuwachukua wafungwa wao wakiwa hai bila mabadilishano na mazungumzo na kukidhi matakwa ya Muqawama".

Abu Obeida

Hamas ilibadilishana mateka 80 wa Israel na wafungwa 240 wa Kipalestina wakati wa usitishaji wa muda wa vita vya Gaza uliomalizika Desemba Mosi. Makubaliano hayo, ambayo yalisimamiwa na Qatar na nchi zingine, yaliruhusu pia kupelekwa misaada ya kibinadamu iliyohitajika sana huko Gaza baada ya wiki kadhaa za mashambulio ya kinyama ya Israel katika eneo hilo.

Duru za utawala wa Kizayuni zinasema Hamas ingali inawashikilia mateka 137 kufuatia operesheni ya Oktoba 7 katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, ambapo walowezi 1,200 wa Kizayuni na vikosi vya kijeshi vya utawala huo ghasibu waliuawa pia.

Jana Jumapili Qatar ilionya kwamba mashambulizi ya mtawalia ya Israel dhidi ya Gaza huenda yakahatarisha mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano katika eneo hilo.

Abu Obeida amesisitiza kuwa Hamas itaendelea kupambana na Israel bila kujali ukubwa wa mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Gaza ambayo amesema yanalenga "kuvunja nguvu ya Muqawama".

Amesisitiza kwa kusema: "hatuna chaguo jengine isipokuwa kupambana na mkaliaji huyu mshenzi wa ardhi katika kila eneo, mtaa na kichochoro," 

Takriban watu 18,000 wameshauawa shahidi huko Gaza katika siku 63 za mashambulizi ya kinyama ya utawala haramu wa Israel, kulingana na takwimu zilizotolewa na maafisa wa wizara ya afya ya Gaza.../

Tags