Rais Pezeshkian: Wairani watajibu chokochoko za maadui dhidi ya nchi yao
(last modified Sun, 27 Oct 2024 03:10:25 GMT )
Oct 27, 2024 03:10 UTC
  • Rais Pezeshkian: Wairani watajibu chokochoko za maadui dhidi ya nchi yao

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian ametoa rambirambi zake kufuatia kuuawa shahidi maafisa usalama wa nchi hii katika mashambulizi ya kichokozi ya jana Jumamosi ya utawala wa Kizayuni na kundi la kigaidi linaloungwa mkono na maajinabi.

Pezeshkian amesisitiza kuwa, taifa la Iran litalipiza kisasi kwa busara na bila woga mkabala wa kitendo chochote cha kipumbavu dhidi ya nchi yao.

Dakta Pezeshkian amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa, "Maadui wa Iran wanapaswa kujua kwamba, taifa hili shupavu linasimama bila woga kutetea ardhi yake na kujibu kitendo chochote cha kipumbavu kwa busara na akili."

"Natoa rambirambi zangu kwa familia na watu wa taifa la Iran kutokana na kuuawa shahidi askari shupavu wa kijeshi na polisi,” ameongeza katika ujumbe wake. 

Matamshi hayo yametolewa baada ya Jeshi la Ulinzi wa Anga la Iran kuzima mashambulizi ya Israel yaliyolenga maeneo ya Tehran na mikoa ya Khuzestan na Ilam.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali uchokozi wa Wazayuni

Jeshi la Iran limesema askari wake wanne waliuawa shahidi katika mashambulizi hayo. Dakta Pezeshkian amewapongeza wahanga hao kwa kusabilia maisha yao kuitetea nchi.

Katika hatua nyingine, jana Jumamosi, maafisa 10 wa polisi waliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi lililofanywa na kundi linaloungwa mkono na mataifa ya kigeni liitwalo Jeish al-Adl huko Goharkoh, mji wa Taftan, katika mkoa wa Sistan na Baluchestan.

Tags