Uongo wa Wazayuni kuhusu takwimu na matokeo ya vita
(last modified Sun, 27 Oct 2024 02:22:32 GMT )
Oct 27, 2024 02:22 UTC
  • Uongo wa Wazayuni kuhusu takwimu na matokeo ya vita

Viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa makusudi na kufuatia kushindwa kukabiliana na oparesheni za kishujaa za makundi ya Muqawama, unaficha ukweli wa mambo kuhusu vita vya Gaza.

Takwimu zilizochapishwa na Wizara ya Vita ya utawala wa Kizayuni wa Israel, ambazo zinajumuisha maafisa wa polisi, maajenti wa Shin Bet (Idara ya Usalama wa Umma) na vikosi vya akiba pia zinaonyesha kuwa zaidi ya askari 10,000 wamejeruhiwa katika vita vya Gaza. Wizara ya Vita ya Israel pia imetoa taarifa ikitangaza kuwa, kuanzia Oktoba 7 mwaka jana hadi sasa wanajeshi, polisi na maajenti ya Shin Bet 890 wameuawa vitani. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, idadi hiyo ni pamoja na maafisa usalama ambao wameuawa huko Gaza katika maeneo ya kaskazini mwa Palestina, kusini mwa Lebanon na katika Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan. 

Utawala wa Kizayuni pia imekiri wazi kuhusu hasara kubwa na kuuawa na kujeruhiwa idadi kubwa ya wanajeshi wake katika mapigano kusini mwa Lebanon. Katika kipindi cha masaa kadhaa yaliyopita takriban wanajeshi 13 wa Israel wameangamizwa katika mapigano ya jeshi ya Israel na wanamuqawama wa Hizbullah kusini mwa Lebanon. Wanamapambano wa Lebanon walikuwa wakisubiri kuwasili wanajeshi hao wa Kizayuni huko "Eita al-Shaab", na baada ya mapigano hayo yaliyoendelea kwa saa kadhaa, waliwaangamiza 13 na kuwajeruhi baadhi yao.

 

Muqawama wa Lebanon Hizbullah ukivurumisha makombora dhidi ya kambi za wanajeshi vamizi wa Israel 

Kutolewa takwimu hizi mpya na Wizara ya Vita ya Israel kunaonyesha kuwa viongozi wa utawala huo wamekuwa wakificha uvamizi na vitendo vya jinai vya jeshi lao na taathira zake tangu kuanza vita vya Gaza.

Kinyume na madai ya maafisa wa Tel Aviv kuhusu vita vya Gaza, kuchapishawa kwa takwimu hizo kunaonyesha kuwa jeshi la Kizayuni linakabiliwa na mgogoro usio na kifani katika masuala ya kijeshi.

Tangu kuanza kwa vita vya Gaza, viongozi wa  Kizayuni pia walikusudia kuibua mazingira ya kueneza habari za uwongo na kukanusha ukweli wa mambo kuhusu vita vya Gaza kwa msaada mkubwa wa  vyombo vya habari vya Marekani na Magharibi kwa ujumla. Vyombo hivyo vya habari vilifuata stratejia mbili za upashaji habari kwa wakati mmoja. Awali, lengo kuu lilikuwa kuzuia kutangazwa habari ambazo zinaweka wazi jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. Lengo jingine la vyombo hivyo vya habari vya Magharibi lilikuwa kujizuia kutangaza habari za mafanikio ya oparesheni za makundi ya mapambano ya ukombozi na Kambi ya Muqawama na vipigo ulivyopata jeshi la utawala wa Kizayuni.

Wanajeshi wa Israel wapata vipigo Ukanda wa Gaza 

Ripoti ya jeshi la utawala wa Kizayuni inaonyesha kuwa mgogoro wa ndani huko Tel Aviv umepanukka hadi ndani ya jeshi la utawala huo; katika hali ambayo hakuna tena njia ya kuficha ukweli wa mambo huku udhaifu, vipigo na hasara wanazopata wanajeshi wa Kizayuni kila uchao katika vita vya Gaza vikiongezeka. 

Hii ni katika hali ambayo kuna tofauti kubwa za kimitazamo kati ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni na Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu; na kuvuja taarifa za kijeshi na kukiri kuhusu suala hilo kunaonyesha kutoridhika pakubwa  makamanda wa jeshi la utawala wa Kizayuni na hali ya mgogoro inayolisibu jeshi la Israel. 

Ongezeko la vifo vya wanajeshi wa jeshi la Kizayuni katika vita vya Gaza na Lebanon ni moja ya matokeo ya uchochezi na hatua za kupenda kujitanua za  Tel Aviv katika eneo hili; jambo ambalo viongozi wa Kizayuni wanalazimika kulikiri waziwazi. Matokeo ya kuendelea vita hivyo yatazidisha idadi ya wanajeshi wa Kizayuni wanaojeruhiwa na kuangamizwa; na wakati huo huo  kambi za kijeshi, za usalama na kijasusi za Israel zitakabiliwa na vipigo visivyoweza kufidiwa. Makundi ya muqawama ya Palestina na muqawama wa Lebanon yametumia vyema nguvu na uwezo wake kukabiliana na jeshi la utawala wa Kizayuni. 

Wanamapambano wa Palestina 

 

Tags