Shughuli katika bandari ya Israel ya Eilat zapungua kwa 80%
Gazeti la Kizayuni la Calcalist limeripoti kuwa, shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo katika bandari ya Eilat ya utawala wa Kizayuni wa Israel zimepungua kwa asilimia 80.
Gazeti hilo limeandika kuwa: Kampuni nyingi zimesimamisha safari za meli kupitia Bahari Nyekundu na Mfereji wa Suez kutokana na tishio (la harakati ya Ansarullah), ambalo limeisababishia hasara kubwa bandari ya Eilat.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, vitisho vya Marekani kwa Yemen vimeshadidisha taharuki katika eneo, na kwamba njia mbadala zinazotumiwa na meli hizo za mizigo kuelekea katika bandari hiyo muhimu ya Wazayuni zimeongeza gharama za usafiri na masafa, na hivyo mizigo inafika kwa kuchelewa.
Vikosi vya Yemen vimeendelea kushambulia kwa makombora meli zinazoelekea bandari za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kabla ya hapo, tovuti ya habari za kiuchumi ya Galobs iliandika kwamba bandari ya Eilat ndiyo iliyopata hasa kubwa zaidi katika vita vya Gaza.

Tovuti hiyo iliripoti kuwa, vita hivyo vimesababisha uharibifu mkubwa kwa bandari ya Eilat na sasa imekaribia kufungwa.
Jeshi la Wanamaji la Yemen limeonya kwamba litaendelea na operesheni za kijeshi dhidi ya meli na maslahi ya adui Mzayuni hadi atakapokomesha hujuma zake dhidi ya Gaza na jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.