Mbali na kuua watoto wachanga, Wazayuni wanafanya uporaji pia Ghaza
Mkuu wa Ofisi ya Upashaji Habari ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa mbali na jinai zao nyingine nyingine kama za kuua watoto wachanga, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wanafanya uporaji pia wa mali za Wapalestina wakati wanapoingia kwenye nyumba walizozivunja kwa mashambulizi ya kikatili na kinyama huko Ghaza.
Televisheni ya Al Mayadeen imemnukuu Ismail Ismail al-Thawabita akisema hayo na kuongeza kuwa, hivi sasa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wanafanya uporaji huo katika nyumba za wakazi wa kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza na wanawalazimisha wakimbizi wa Palestina kuwapa kila walicho nacho kwa kutumia mitutu ya bunduki.
Amesema kuna karibu wakimbizi milioni moja wa kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza na wanaishi kwenye mazingira magumu sana huku wakikabiliwa na majanga mbalimbali ya kibinadamu.
Mkuu huyo wa Ofisi ya Upashaji Habari ya HAMAS ameongeza kuwa, hospitali za Ghaza hazina uwezo tena wa kupokea majeruhi na wameitaka Misri na nchi nyingine za Kiarabu kukubali kupokea majeruhi wa Palestina.
Vile vile ametoa mwito wa kufunguliwa haraka kivuko cha Rafah na vivuko vingine vya kuingia na kutoka Ghaza huku akisema kuwa, utawala wa Kizayuni unaendelea kuwashambulia wahudumu wa afya, mahospitali na vituo vingine vya matibabu gha Ukanda wa Ghaza.
Kabla ya hapo, Ashraf al Qadar, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Palestina huko Ghaza alikuwa amesema kuwa, Hospitali ya al 'Uda ya eneo la Jabalia huko kaskazini mwa Ghaza imezingirwa na wanajeshi makatili wa Israel tangu tarehe 5 Disemba hadi hivi sasa.
Amesisitiza kuwa, hakuna chochote kinachoingia kwenye hosptali hiyo kutokana na mzingiro huo wa wanajeshi Wazayuni, si chakula, si maji na si chochote; wakati ndani ya hospitali hiyo mna wagonjwa takriban 240 hivi sasa.