Mpango wa amani wa Yemen kusainiwa mwezi ujao nchini Saudia
Mpango wa amani wa Yemen unatazamiwa kusainiwa mwanzoni mwa mwezi ujao wa Januari, 2024 nchini Saudi Arabia.
IRNA imenukuu ripoti ya shirika la habari la Sputnik la Russia inayosema kuwa, hafla ya kusaini ramani ya njia ya amani ya Yemen itafanyika mwezi ujao mwakani katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudia.
Vyanzo vya habari vinaarifu kuwa, Umoja wa Mataifa, Saudi Arabia na Oman zinafanya juu chini kwa ajili ya maandalizi ya kusainiwa mpango huo wa amani ya Yemen.
Habari zaidi zinasema kuwa, serikali ya Saudi Arabia imeafiki kusimamia mishahara ya mwaka mmoja ya wafanyakazi wote wa serikali ya Yemen.
Aidha imeafikiwa kuwa, mauzo ya mafuta na gesi ya Yemen nje ya nchi itaanza tena kwa lengo la kujaribu kuukwamua uchumi wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amesema pande hasimu nchini Yemen zimekubali kuchukua hatua za kivitendo za kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita.
Sputnik imemnukuu Hans Grundberg akisema kuwa, "Tunakaribisha irada ya pande zote husika ya kuchukua hatua za kutekeleza usitishaji vita wa nchi nzima, kuboresha hali za maisha za Wayemen, na kushiriki kwenye mchakato jumuishi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa."