Televisheni ya CNN yatuhumiwa kuchuja habari zote zinazohusiana na Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106844-televisheni_ya_cnn_yatuhumiwa_kuchuja_habari_zote_zinazohusiana_na_gaza
Tovuti ya The Intercept imetangaza kwamba, habari zote ambazo mtandao wa habari wa CNN unaangazia kuhusu vita vya Ukanda wa Gaza huchujwa na kudhibiitiwa na jeshi la Israel kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
(last modified 2026-06-17T03:32:54+00:00 )
Jan 05, 2024 07:27 UTC
  • Televisheni ya CNN yatuhumiwa kuchuja habari zote zinazohusiana na Gaza

Tovuti ya The Intercept imetangaza kwamba, habari zote ambazo mtandao wa habari wa CNN unaangazia kuhusu vita vya Ukanda wa Gaza huchujwa na kudhibiitiwa na jeshi la Israel kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

The Intercept imefichua katika ripoti yake kwamba habari zote zinazohusu Gaza zinazotayarishwa na wanahabari wote wa CNN popote pale wanapokuwa duniani lazima kwanza zipelekwe kwenye ofisi ya chombo hicho cha habari huko Jerusalem kabla ya kuchapishwa au kutangazwa.

The Intercept inasema, ingawa CNN inadai kuwa madhumuni ya sera hii ni kuhakikisha usahihi wa ripoti zake, lakini maana ya sera hii kiutendaji ni kwamba sehemu kubwa ya utangazaji wa habari wa CNN hutengenezwa na waandishi habari ambao wanapaswa kuzingatia sheria za udhibiti na uchujaji wa habari za jeshi la Israel.

Kulingana na Intercept, katika ofisi ya CNN mjini Jerusalem, jeshi la Israel, pamoja na kubainisha mada ambazo hazipaswi kuripotiwa, linaweza kuzuia uchapishaji au utangazaji wa makala ambayo linaona kuwa hayafai.

The Intercept pia iliripoti mwezi uliopita kwamba jeshi la Israel hivi karibuni liliainisha masuala manane ambayo utangazaji wake unapaswa kuwekewa mipakka na vikwazo.

Nusu ya waliouawa na Israel Ukanda wa Gaza ni watoto wadogo

Mfanyakazi wa mtandao wa habari wa CNN ameiambia Intercept kwa sharti la kutotajwa jina kwamba maudhui mbalimbali zinazotangazwa na televisheni hiyo mashuhuri ya Marekani mara nyingi huhaririwa kwa hila maalumu ili ziwe karibu na simulizi ya serikali ya Israel.

Zaidi ya Wapalestina 22,000 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 57,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza tangu tarehe 7 Oktoba.

Mashambulizi hayo ya kikatili yanafanyika kwa kutumia silaha na mabomu yanayotolewa na Marekani kwa utawala huo katili.