Wazayuni wazidi kupapurana; Netanyahu chagua moja!
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106876-wazayuni_wazidi_kupapurana_netanyahu_chagua_moja!
Mzozo unazidi kurindima ndani ya baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni huku Benny Gants akimshambulia kwa maneno makali waziri mkuu wa utawala huo katili, Benjamin Netanyahu akimwambia achague moja, imma kuweko kwenye serikali ya muungano au kulinda usalama wa ndani ya Israel.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jan 06, 2024 04:09 UTC
  • Wazayuni wazidi kupapurana; Netanyahu chagua moja!

Mzozo unazidi kurindima ndani ya baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni huku Benny Gants akimshambulia kwa maneno makali waziri mkuu wa utawala huo katili, Benjamin Netanyahu akimwambia achague moja, imma kuweko kwenye serikali ya muungano au kulinda usalama wa ndani ya Israel.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Anadolu ambalo limemnukuu Benny Gants akimshambulia vikali Netanyahu na kumlaumu kwa kushindwa kukabiliana ipasavyo na operesheni za Kimbunga cha al Aqsa.

Vilevile amemlaumu Netanyahu kwa kumshamblia mkuu wa jeshi la utawala wa Kizayuni na kusema kuwa, waziri mkuu huyo wa Israel amefanya hivyo kujinufaisha kisiasa na kwamba sasa ana moja ya machaguo mawili, imma kuwa na serikali ya muungano au kulinda usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni.

Netanyahu ameelemewa na mashambulizi makali kutoka kwa wajumbe wa baraza lake la vita kufuatia mzozo mkubwa uliozuka kwenye kikao cha baraza lake la vita hasa dhidi ya kuundwa kamati maalumu ya kuchunguza sababu za kufeli jeshi la Israel kwenye operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa. 

 

Benny Gants amesema, kitendo cha Netanyahu cha kumshambulia mkuu wa jeshi la Israel hakitoweza kumsaidia kisiasa na amemtaka aache kutanguliza chama na masuala yake binafsi mbele ya utawala wa utawala wa Kizayuni.

Benny Gants vile vile amesema, hivi sasa Israel imo kwenye vita vigumu mno katika historia yake yote. Inaendesha vita katika medani kadhaa hivyo si sahihi kuzozana Wazayuni wenyewe kwa wenyewe na kutupiana lawama kutokana na kufeli kwao kwenye vita.

Hii ni mara ya kwanza kwa mjumbe huyo wa baraza la mawaziri la kivita la Israel kutoa maneno makali kwa waziri mkuu wa Israel tangu tarehe 7 Oktoba 2023 alipojiunga na serikali hiyo ili kuisaidia kufanya jinai dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza. Vipigo vya mtawalia wanavyopata Wazayuni kwenye medani za vita vimezusha mgogoro na mzozo mkubwa ndani ya utawala wa Kizayuni.