Ansarullah: Hizbullah ya Lebanon imeutia nguvu sana muqawama wa Palestina
Mohammad Abdus Salaam, Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeutia nguvu sana muqawama wa Palestina hasa kwenye Ukanda wa Ghaza kutokana na kuushughulisha kwa mashambulizi utawala wa Kizayuni katika mipaka ya Lebanon.
Abdus Salaam amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema hayo jana usiku na kuongeza kuwa, opereshenei za kijeshi za muqawama wa Kiislamu wa Lebanon kwenye maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel ni sehemu muhimu ya kuwaunga mkono kivitendo Wapalestina na kujitolea muhanga sana katika kadhia hiyo kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu.
Matamshi hayo ya Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen yametolewa katika hali ambayo, vyombo vya habari vimeripoti kufanyika wimbi jipya la mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Hizbullah ya Lebanon dhidi ya kambi muhimu ya kijeshi ya Israel, kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa, imeitwanga kambi ya kijeshi ya al Rahim ya utawala wa Kizayuni kwa kutumia makombora ya Burkan.
Vyombo vya habari vimeonesha picha na mikanda ya video inayoonesha jinsi kambi hiyo ya kijeshi ya Israel inavyoteketea kwa moto baada ya kushambuliwa ha Hizbullah ya Lebanon.
Wakati huo huo Brigedi za Quds, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina zimetangaza kuwa kwa mara nyingine imevitwanga kwa makombora vitongoji vya walowezi wa Kizayuni karibu na Ukanda wa Ghaza.
Taarifa hiyo ya Brigedi za Quds imesema, vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya Sdirot Nir'am na vinginevyo vinavyopakana na Ukanda wa Ghaza vimepigwa kwa makombora kadhaa ya Jihadul Islami Jumatatu usiku.