Hamas: Israel imeshindwa kufikia malengo ya vita huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107016-hamas_israel_imeshindwa_kufikia_malengo_ya_vita_huko_gaza
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesema utawala haramu wa Israel umeshindwa kufikia malengo yake yoyote baada ya takriban siku 100 za vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-01-10T01:08:14+00:00 )
Jan 10, 2024 01:08 UTC
  • Hamas: Israel imeshindwa kufikia malengo ya vita huko Gaza

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesema utawala haramu wa Israel umeshindwa kufikia malengo yake yoyote baada ya takriban siku 100 za vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Ameongeza kuwa utawala huo wa Kizayuni umedhihirisha tu asili yake ya "kiu ya damu na mauaji" kwa ulimwengu mzima kwa kufanya mauaji ya kila aina katika eneo lililozingirwa.

Ismail Haniyeh aliyasema hayo katika kongamano la Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS) katika mji mkuu wa Qatar wa Doha siku ya Jumanne, akibainisha kuwa kusimama kideite na istikama ya wakazi wa Gaza imeizuia Israel kufikia malengo yake.

Haniyeh amesema:"Malengo yaliyotangazwa ya vita dhidi ya Gaza ni kuondoa Harakati ya Hamas, kuwarejesha wafungwa wao (wanaoshikiliwa na Hamas) na kutekeleza mpango wa kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza."

Mkuu huyo wa Hamas alisisitiza zaidi kwamba harakati ya Hamas haiwezi kuondolewa kwa sababu ipo katika nyoyo za Wapalestina wote na pia katika nyoyo za Umma wa Kiislamu na watu huru duniani.

Haniyeh aidha amesema njia pekee ya kuwaachilia wafungwa wa kivita wa Israel wanaoshikiliwa Gaza ni kuachiliwa huru mateka Wapalestina wanaoshikiliwa katika vizuizi vya Israel.

Mtaa ulioharibiwa kwa mabomu ya Israel huko Gaza

Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina  kwenye Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya Hamas kutekeleza operesheni ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya utawala huo wa Kizayuni ikiwa ni kulipiza kisasi kwa ukatili wa utawala huo  dhidi ya watu wa Palestina.

Hadi sasa utawala wa Israel imewauwa Wapalestina wasiopungua 23,084 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine 58,926.

Maelfu zaidi pia wametoweka na wanaodhaniwa wamekufa chini ya vifusi katika Ukanda wa Gaza, ambao umezingirwa kikamilifu na Israel.