UNRWA yasema Gaza haikaliki tena kutokana na hujuma ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107052-unrwa_yasema_gaza_haikaliki_tena_kutokana_na_hujuma_ya_israel
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) linasema Ukanda wa Gaza sasa ni "mahali pasipoweza kukaliwa na wanadamu" huku Israel ikiendelea na vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo linaozingirwa la Palestina.
(last modified 2024-01-10T08:33:57+00:00 )
Jan 10, 2024 08:33 UTC
  • UNRWA yasema Gaza haikaliki tena kutokana na hujuma ya Israel

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) linasema Ukanda wa Gaza sasa ni "mahali pasipoweza kukaliwa na wanadamu" huku Israel ikiendelea na vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo linaozingirwa la Palestina.

Msemaji wa UNRWA Adnan Abu Hasna amesema Gaza ni sehemu mbaya zaidi duniani, na eneo hilo limegeuzwa kuwa sehemu isiyoweza kukaliwa na wanadamu huku kukiwa na ripoti kwamba vita vya Israel vimesababisha nyumba nyingi za Gaza kuwa magofu.

Kwa sasa kuna watu milioni 1.9 waliokimbia makazi yao kote Gaza, na miongoni mwao karibu milioni 1.4 wamepata hifadhi katika shule 155 zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Abu Hasna pia amesema kuwa wakazi wengi wa Gaza wanalazimika kukimbilia mji wa kusini wa Rafah karibu na mpaka na Misri.

Aidha ameonya kwamba uhamisho wa wakazi wote wa Gaza hadi Rafah unazidi uwezo uliopo wa kutoa msaada kwao, akibainisha, "UNRWA haiwezi kukabiliana na mporomoko unaoendelea."

Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya Hamas kutekeleza operesheni ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya utawala huo wa Kizayuni ikiwa ni katika kulipiza kisasi kwa ukatili wa utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.

Hadi sasa utawala wa Israel imewaua Wapalestina wasiopungua 23,300 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine 59,000.

Maelfu zaidi pia wametoweka na wanadhaniwa wamekufa chini ya vifusi katika Ukanda wa Gaza, ambao umezingirwa kikamilifu na Israel.