Jeshi la Yemen laipiga kwa mizinga na droni meli ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107070-jeshi_la_yemen_laipiga_kwa_mizinga_na_droni_meli_ya_marekani
Msemaji rasmi wa Jeshi la Yemen ametangaza kuwa, vikosi vya nchi hiyo vya majeshi ya majini na ya droni (ndege zisizo na rubani) vimefanya operesheni ya pamoja ya kupiga kwa makombora meli ya Marekani katika Bahari ya Sham (Bahari Nyekundu).
(last modified 2024-01-11T00:39:27+00:00 )
Jan 11, 2024 00:39 UTC
  • Jeshi la Yemen laipiga kwa mizinga na droni meli ya Marekani

Msemaji rasmi wa Jeshi la Yemen ametangaza kuwa, vikosi vya nchi hiyo vya majeshi ya majini na ya droni (ndege zisizo na rubani) vimefanya operesheni ya pamoja ya kupiga kwa makombora meli ya Marekani katika Bahari ya Sham (Bahari Nyekundu).

Televisheni ya Al Masirah ya Yemen imemnukuu Brigedia Jenerali Yahya Sarii, akitangaza habari hiyo jana na kuongeza kuwa, vikosi vya baharini na makombora pamoja na vile vya droni vya jeshi la Yemen vimeendesha kwa mafanikio operesheni hiyo dhidi ya meli ya Marekani.

Amesema, operesheni hiyo imelenga meli ya Marekani iliyokuwa inapeleka misaada kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kabla ya jambo lolote, operesheni hiyo ni majibu kwa jinai za jeshi la Marekani za kushambulia wanajeshi wa Yemen na kuua shahidi wanajeshi 10 wa jeshi la majini la nchi hiyo ya Kiarabu.

Operesheni ya jeshi la Yemen ya kuteka meli ya utawala wa Kizayuni katika Bahari Nyekundu

 

Brigedia Jenerali Yahya Sarii ameongeza kuwa, tutaendelea kupambana na vitisho vyovyote vinavyotoka kwa adui; na hiyo ni haki yetu, kwani ni katika kulinda nchi yetu, na kuwalinda wananchi wetu na umma mzima wa Kiislamu. Hatutosita hata kidogo kuchukua hatua za kivitendo katika njia hiyo.

Vile vile amesema, meli yoyote inayoelekea kwa utawala wa Kizayuni wa Israel haitoruhusiwa kupita kwenye Bahari ya Sham na katika Lango Bahari la Bab al Mandab hadi pale Israel itakapokomesha jinai zake dhidi ya Wapalestina na kuondolewa kikamilifu mzingiro wa Ghaza.

Msemaji huyo rasmi wa jeshi la Yemen amebainisha wazi msimamo usiotetereka wa nchi hiyo ya Kiislamu akisema: Tunatangaza hadharani kwamba meli nyingine zote zinaruhusiwa kupita kwenye maji yetu isipokuwa meli ambazo zinaelekea kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.