Muqawama: Tuko pamoja na Yemen, amani haitopakana mpaka Quds ikombolewe
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na makundi mbalimbali ya muqawama ya Palestina, Lebanon na Iraq yametoa matamko na kulaani vikali mashamblizi ya Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen na kusisitiza kuwa yako pamoja na wananchi wa Yemen na wataendelea kushirikiana hadi Quds itakapokombolewa.
Alfajiri ya leo Ijumaa, Marekani na Uingereza zimefanya mashambulizi 73 dhidi ya maeneo tofauti ya Yemen kutokana na taifa hilo la Kiislamu na Kiarabu kuwa na msimamo usiotetereka wa kuwaunga mkono ndugu zao Wapalestina.
Mara baada ya mashambulizi hayo, harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kuwa imeanza kujibu mashambulizi hayo kwa kushambuliwa meli za kivita za Marekani na Uingereza kwenye Bahari Nyekundu (Bahari ya Sham).
Katika radiamali na mjibizo wake wa kwanza baada ya mashambulizi ya Marekani na Uingereza huko Yemen, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan’ani amesisitiza kuwa, mashambulio ya kiholela kama hayo yatazidisha tu wasiwasi na ukosefu wa utulivu kwenye eneo hili.
Kwa upande wake shirika la habari la FARS limezinukuu harakati za muqawama na mapambano ya Kiislamu yaani Hizbullah ya Lebanon, HAMAS na Jihadul Islami za Palestina, Kataib Sayyidush Shuhada na Asaib Ahlul Haq za Iraq pamoja na chama cha Al Tayyar al Shaabi cha Tunisia zikitoa matamko tofauti ya kulaani jinai hizo za Uingereza na Marekani huko Yemen.
Leo Ijumaa, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imenukuliwa na televisheni ya Al Manar ikisema katika sehemu moja ya taarifa yake kwamba, Hizbullah inalaani vikali uvamizi wa waziwazi wa Marekani na Uingereza nchini Yemen; Yemen ambayo imesimama kwa nguvu zake zote na kuwajibika kikamilifu katika kuwahami wananchi wa Palestina na muqawama wao usiotetereka.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema mashambulio ya Marekani na Uingereza nchini Yemen ni ugaidi wa wazi na yatashadidisha tu mgogoro kwenye eneo hili.
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina nayo imelaani uhalifu huo wa Marekani na Uingereza na kusema kuwa, hauwezi kuficha kushindwa utawala wa Kizayuni katika vita vya Ghaza.
Harakati ya Kataib Sayyidush Shuhada ya Iraq imesema kwenye taarifa yake kuwa utawala wa Kizayuni na Marekani ndio wahatarishaji wakuu wa usalama na amani Asia Magharibi na kama mizizi yao haitang'olewa na kukombolewa Quds Tukufu, basi amani haitopakana kwenye eneo hili.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Harakati ya Asaib Ahlul Haq ya Iraq, Sheikh Qeis al Khaz'ali amelaani mashambulio hayo ya Marekani na Uingereza nchini Yemen na kusema kuwa nchi hizo za kiistikbari zinafanya juhudi za kipuuzi kwani mashambulizi hayo hayatousaidia chochote utawala wa Kizayuni ghairi ya kuhatarisha zaidi tu usalama wa eneo hili.
Kwa upande wake chama cha Al Tayyar Al Shaabi cha Tunisia kimelaani mashambulio ya Marekani na Uingereza huko Yemen na kusema kuwa, mashambulizi hayo yamethibitisha kwamba Israel ni kituo kikuu cha kulinda malengo ya kibeberu ya Magharibi kwenye eneo hili.