Sayyid Nasrullah: Taarifa zetu zinathibitisha kuangamizwa Wazayani katika kituo cha Meron
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa harakati hiyo ya Muqawama imerusha roketi 62, yakiwemo maroketi 20 ya Katyusha na makumi ya makombora ya Kornet yenye uwezo mpya, ambayo yamelenga shabaha huko Meron, kaskazini mwa Israel, na kwamba filamu iliyorushwa mitandaoni na Hizbullah haifichui ukweli wote.
Sayyid Nasrullah ameyasema hayo leo katika hotuba yake katika kumbukumbu ya wiki moja baada ya kuuawa shahidi Kamanda Wissam Tawil (Hajj Jawad) katika mji wa kusini mwa Lebanon wa Khirbet Selm na kuongeza kuwa: "Ni lazima tushirikiane kutayarisha sababu zote za kusimama imara katika vita hivi kwa sababu hatujui vitaendelea mpaka lini."
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: Siku 100 zimepita na Gaza inaendelea kupigana kwa ujasiri usio na kifani katika historia, na Muqawama wa Gaza, katika mirengo yake yote, unapigana usiku na mchana kwa ushujaa usio na mfano.
Sayyid Nasrullah amesema wafuatiliaji wengi wa vita vya Kimbunga cha Al-Aqsa wanakubali kwamba "Israel" imezidisha usiri na udhibiti wa habari kuliko hapo awali akisisitiza kwamba adui Mzayuni ameshindwa kufikia malengo yake yaliyotangazwa.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa: Baadhi ya vyombo vya habari vya maadui vinasema askari 4,000 wa Israel wamepata ulemavu, jambo ambalo lina maana kwamba wametoka nje ya utumishi wa jeshi, na kwamba huenda idadi hiyo ikafika 30,000, lakini janga kubwa zaidi litakuwa pale vita vitakapomalizika na ukubwa wa maafa yaliyoipata Israel kutokana na vipigo vya kambi ya Muqawama, utakapofichua.
Amesema, kila siku kuna maafa katika upande wa adui huko Gaza, katika kukabiliana na wanamuqawama wa Lebanon na Ukingo wa Magharibi.